The House of Favourite Newspapers

Coutinho atimuliwa Yanga

0

ANDREYCOUTINHOKiungo mshambuliaji wa Yanga, Andrey Coutinho.

Khadija Mngwai, Dar es Salaam
SASA yametimia, ndivyo unavyoweza kusema kwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Andrey Coutinho kufuatia hatua ya kufungashiwa virago vyake klabuni hapo huku nafasi yake ikitarajiwa kuzibwa na kiungo kutoka nje ya nchi.

Coutinho aliingia katika mvutano wa siku nyingi na uongozi wa klabu hiyo ambapo wapo waliokuwa wakimhitaji na wapo waliokuwa wakimkataa huku akiwa siyo chaguo la kocha, Hans van Der Pluijm kufuatia kumuweka benchi.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, alifunguka kuwa, tayari uongozi wa klabu hiyo umeshavunja mkataba wa miezi nane uliokuwa umebakia huku wakiwa katika mazungumzo na mchezaji mwingine kutoka nje ya nchi, kwa lengo la kuziba nafasi yake.

“Tangu awali nilieleza kuwa hatutasajili hadi atakapoondoka mtu, hivyo tayari tumeshaachana na Coutinho. Tunafanya mazungumzo na mchezaji kutoka nje ya nchi kuweza kuziba nafasi yake, japokuwa siwezi kuweka wazi ni nchi gani.

“Moja ya sababu zilizofanya tuachane naye ilikuwa ni hili la kuchelewa kurudi, japokuwa zipo sababu nyingine ambazo zimesababisha kufikia hatua ya kuachana naye.

“Alibakisha mkataba wa miezi nane, hivyo tumemalizana naye kwa kumlipa kila kitu na hatudaiani naye, tunaamini mchezaji tutakayemsajili atakuwa na kiwango kizuri cha kuweza kuziba nafasi yake ambaye atatua kabla ya Desemba 15 dirisha kufungwa,” alisema Tiboroha ambaye hakuwa tayari kuweka wazi wamemlipa kiasi gani, hata hivyo taarifa nyingine zinadai kuwa amelipwa Sh milioni 30.

Kwa upande wake Coutinho, amemwambia mwandishi wetu, Sweetbert Lukonge kuwa, anatarajia kuondoka nchini leo Jumatatu kurudi kwao Brazil akajipange upya baada ya kusitishiwa ulaji na Yanga.

“Nitaimisi sana Tanzania,” alisema Coutinho alipozungumza kwa ufupi na mwandishi wetu.

Leave A Reply