Cristiano! Fundi wa Soka Anayezeeka na Utamu Wake

 

MSHAMBULIAJI yota wa klabu ya soka ya Juventus Cristiano Ronaldo, leo 5/2/2021 anatimiza miaka 36 tangu kuzaliwa kwake.

 

 

Ronaldo aliyezaliwa Februari 5, 1985k katika mji wa Madeira, Ureno, amekuwa mmoja wa wachezaji wenye mafanikio makubwa sana katika historia ya mchezo wa soka duniani tangu alivyoanza rasmi soka la ushindani katika klabu ya Sporting CP ya nyumbani kwao mwaka 2003.

 

 

Alianza kufanikiwa kimataifa zaidi alivyojiunga na Manchester United mwaka huohuo wa 2003 na kudumu kwa miaka sita. Alifanikiwa kufanya makubwa kwa kutwaa vikombe mbalimbali vya ligi za ndani pia kutwaa ubingwa wa ligi ya mabingwa Ulaya (UEFA) mwaka 2008, pia alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Dunia ”Ballon d’Or”.

 

 

Ronaldo alihamia klabu ya Real Madrid mwaka 2009 na kutambulisha ‘ufalme’ wake, kwa kufanya vizuri kama timu na yeye binafsi alifanikiwa zaidi kutwaa vikombe mbalimbali hasa kwenye ligi ya mabingwa wa Ulaya mara nne katika uwepo wake Madrid kwa miaka takribani kumi ambapo ilikuwa mwaka 2013-14, 2015-16,2016-17 na 2017-18.

 

 

Mwaka 2018, Ronaldo alihamia klabu ya Juventus kwa uhamisho ulioshtua dunia, wengi wakimtaja kuwa mzee na amekwisha kiuchezaji kutokana na umri wa miaka 33 aliyokuwa nayo lakini huko nako alipata mafanikio ya kutosha ikiwemo ubingwa mara mbili mfululizo wa ligi ya Italia.

 

Takwimu za Ronaldo zinaonesha ameifungia Sporting CP magoli 5 katika michezo 31, Manchester United magoli 118 katika michezo 292, Real Madrid magoli 450 katika michezo 438 na Juventus magoli 87 katika michezo 112, pia ameweza kumudu kufunga magoli zaidi ya 300 akiwa amefikisha umri wa miaka 30.

Toa comment