The House of Favourite Newspapers

CUF Kutoa tamko kuhusu kurudiwa uchaguzi Zanzibar

0

Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi (CUF), leo linatarajia kutangaza uamuzi mzito kutokana na kikao cha Kamati ya Utendaji, kilichofanyika jana jijini Dar es Salaam chini ya Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji kilifanyika kwa saa tatu kujadili suala la tarehe iliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya kurudia uchaguzi wa Zanzibar, uliofutwa Oktoba 28, mwaka jana.
Kamati hiyo ambayo ilikuwa na ajenda moja pekee, ilijadili na  kutoa uamuzi mzito ambayo yatawasilishwa kwenye Baraza Kuu leo na kutolewa kwa umma.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ambaye hakutaka kutajwa jina , alisema kuwa maazimio yaliyotolewa na kikao hicho kilichoanza saa nne asubuhi, yataishangaza dunia.
Alisema uchaguzi uliotangazwa na ZEC kuwa utafanyika  Machi 20, mwaka huu, ni batili kwa kuwa tayari mshindi wa uchaguzi huo anafahamika ni Maalim  Seif.
“Jukumu kubwa la kikao cha Kamati Tendaji kwa mujibu wa Katiba (ya CUF) ni kuandaa ajenda kwa ajili ya kikao cha Baraza Kuu litakaloanza kesho (leo) na baada ya hapo tutatangaza msimamo wetu juu ya uchaguzi huo,” kilieleza chanzo hicho.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa CUF, Silas Bwire, Kamati ya Utendaji ilikuwa na wajumbe 18 kutoka Tanzania Bara na  Zanzibar, ambao ni viongozi waandamizi wa chama.
Baraza kuu ambalo linatarajia kufanya kikao chake leo, litakalopokea ajenda zilizojadiliwa jana, lina wajumbe 60.
Kikao cha Baraza ambacho kitaongozwa na Mwenyekiti wake, Dk. Twaha Tasilima, kitajadili kwa kina ajenda zitakazowasilishwa pamoja na kuzitolea uamuzi.

Wakati hatima ya CUF kushiriki au kutoshiriki uchaguzi wa marudio inatarajia kufahamika leo, mgawanyiko mkubwa umeibuka miongoni mwa wajumbe wake wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa.

Katika mgawanyiko huo, wamo wanaopinga kushiriki huku wengine wakitaka chama kuangalia upya msimamo wa kususia uchaguzi huo.

Akizungumzia mgawanyiko huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano  wa  CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema kutokana na ukubwa na uzito wa mgogoro wa uchaguzi, mgawanyiko ni jambo ambalo halikwepeki kwa chama kikubwa kama hicho.

Alisema uongozi wa chama uko makini katika kujadili ajenda ya mgogoro wa uchaguzi na kuwataka viongozi na wanachama pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa na moyo wa subira wakati Baraza Kuu la Uongozi la Chama linajiandaa kutoa kauli ya mwisho juu ya hatima ya uchaguzi huo.
Jussa alisema uamuzi utakaotolewa na Baraza Kuu ndio utakuwa mwongozo kwa wagombea wote wa chama pamoja na wanachama na watu wanaokiunga mkono chama.
Alisema mchezo aliyoufanya Jecha wa kufuta matokeo ya uchaguzi kwa manufaa ya CCM, haukubaliki katika misingi ya demokrasia na utawala bora.
Leave A Reply