Na Ibrahim Mussa | CHAMPIONI |GPL
BAADA ya kuchanika juu ya jicho, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva amejikuta akiangusha kilio kutokana na jeraha alilopata kwani atakosa mechi mbili zilibakia ambazo ni sawa na dakika 180.
Msuva alipata majeraha hayo katika mchezo wa juzi Jumamosi dhidi ya Mbeya City wakati anafunga bao la kwanza kwenye ushindi walioupata wa mabao 2-1 na kumfanya kuwa juu kwenye orodha ya ufungaji akiwa na mabao 14.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Msuva alisema kuwa licha ya kuongoza kwa mabao lakini anaamini nafasi yake ya kucheza mechi zilizobaki ni ndogo kutokana na jeraha alilopata kitu ambacho kinamuumiza kufikia malengo yake.
“Kiukweli nimeumia, dokta ndiyo anafahamu zaidi lakini maumivu ninayosikia ni makubwa kwa sababu nimeshonwa nyuzi sita na sitaweza kulazimisha kucheza mechi zilizobaki, naangalia hali yangu kwanza itakuwaje.
“Ligi imebadilika na imekuwa ngumu sana msimu huu, changamoto ya ushindani ilikuwa kubwa kwa wafungaji wenzangu na kuna kitu nimejifunza, ingawa bado naumia kukosa mechi hizo kwa sababu mipango yangu ya ufungaji bora imeishia njiani, hivyo lolote linaweza kutokea,” alisema Msuva.
Daktari wa timu hiyo, Edward Bavu, amesema: “Msuva hataweza kucheza mechi zilizobaki kwa sababu ya jeraha, maana amepata ‘cut warms’ juu ya jicho la kushoto na tumemshona nyuzi sita.”