The House of Favourite Newspapers

Daktari Achambua Ugonjwa wa Mbowe

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

BAADA ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kulazwa Hospitali ya Muhimbili kwa saa 24, madaktari waliozungumza na gazeti hili juzi (Jumatano) wamechambua hali za kiafya alizozielezea kiongozi huyo kuwa zilichangia kuugua kwake.

Mbowe baada ya kutoka hospitali alikolazwa alisema, msongo wa mawazo, kazi nyingi na uchovu wa kukosa usingizi vilisababisha aanguke ghafla na baadaye alazwe Muhimbili.

Akichambua ugonjwa wa msongo wa mawazo, Dk Marise Richard ambaye amekuwa akihudumu katika hospitali mbalimbali za serikali nchini ikiwemo ya Mwananyama alilieleza gazeti hili kwamba mtu unapokuwa na msongo wa mawazo kitaalamu ‘stress,’ mwili hutengeneza kwa wingi homoni aina ya ‘adrenaline’ na ‘cortisol.’

“Kazi yake kuu homoni hizo ni kuitayarisha ama kukabiliana na kitu ambacho kwa wakati huo kinaonekana kitaamsha mihemko. Adrenaline inafanya moyo wa mtu ufanye kazi kwa nguvu zaidi, ili kuweza kusukuma damu kwa wingi hasa katika misuli, ubongo na kwingine, hivyo basi itaongeza mapigo ya moyo na msukumo wa damu kwa ujumla.

“Homoni aina ya Cortisol, kazi yake ni kuutayarisha mwili kwa kuongeza sukari kwenye damu ili sukari hii ikatumike kutengeneza nishati yaani energy ambayo utaihitaji sana katika kipindi hicho.

“Hivyo basi, itahusika kukiamuru kiungo cha ini, ambacho mojawapo ya kazi zake ni kuhifadhi glucose (sukari) katika hali ya glycogen.

“Italiamuru ini kuitoa hiyo glycogen na ibadilishwe haraka kuwa ‘glucose’ na ‘glucose’ ndiyo inayotumika kutengeneza nguvu au nishati na kusababisha kuongezeka sukari katika damu.

“Sukari ambayo itakuwa imetoka kwenye kuhifadhiwa katika ini huongeza sukari katika damu itakayoenda katika seli na kusababisha kuongeza nguvu. Hii ni hali ya kawaida katika miili yetu.

“Mtu mwenye ugonjwa wa moyo au kisukari anashauriwa sana ajitahidi kuepuka ‘stress’ zilizopitiliza au ili kuuzuia mwili wake kutengeneza kila mara kwa wingi hizi homoni za adrenaline na cortisol.

“Zinapozidi, husababishia mtu kupata msongo wa mawazo katika akili yake,” alifafanua Dk Richard.

Aliongeza kuwa msongo wa mawazo huathiri akili na mgonjwa huhitaji matibabu ya kitaalamu kwa sababu huwa unaharibu mpangilio mzuri wa fikra katika ubongo na kuharibu utaratibu mzima wa ubongo na hasa katika sehemu zinazohusika na hisia, mihemko na kumbukumbu.

Naye Dk. Godfrey Chale alisema kama Mbowe alikosa usingizi kwa siku nyingi ulichangia kwa kiasi kikubwa kuharibu afya ya akili na mishipa ya fahamu na kukosa usingizi kitaalamu huitwa insomnia, kitu ambacho mtu huishiwa nguvu na kudhoofika.

“Kiafya mwanadamu anashauriwa kupata muda wa kulala na kuweza kupumzisha akili, kwa wale wa umri wa kuanzia miaka 18 hadi miaka ya 60 wanashauriwa kulala kwa muda wa saa zisizopungua nane na muda huo huongezeka kadri mtu anavyozeeka,” alisema Dk Chale.

Hata hivyo, alisema kuhisi uchovu wa kila siku na mara kwa mara huweza kuwa pia ni kiashiria cha ugonjwa wa kisukari au huenda ikawa ni dalili ya matatizo ya moyo, ambapo alimshauri Mbowe kuwa karibu na madaktari ili apate ushauri, vipimo na tiba sahihi ya tatizo lake.

STORI: Mwandishi Wetu, IJUMAA

Comments are closed.