Daktari Ampa Ruhusa Msuva Kucheza

Kiungo wa Yanga, Simon Msuva.

MUSA MATEJA | CHAMPIONI |HABARI

LICHA ya kushonwa nyuzi sita wikiendi iliyopita, kiungo wa Yanga, Simon Msuva, huenda akaonekana uwanjani katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC, hiyo ni kwa mujibu wa daktari wa timu hiyo, Edward Bavu.

Msuva alipata majeraha ya kuchanika juu ya jicho wakati anafunga bao la kwanza kwenye mchezo wao dhidi ya Mbeya City uliomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, Jumamosi iliyopita.

Baada ya kupata majeraha hayo, Msuva alishonwa nyuzi sita na kutakiwa kukaa nje ya uwanja kwa siku saba hali iliyosababisha aukose mchezo wao wa Jumanne dhidi ya Toto Africans.

Bavu ameliambia Championi Ijumaa kuwa, Msuva anaweza kucheza mchezo wa mwisho kwa sababu anatarajiwa kutolewa nyuzi hizo leo Ijumaa.

“Uvimbe wake umepungua sana na hali yake inaendelea vizuri, hivyo kesho (leo), tunaweza kumtoa nyuzi na ataungana na wenzake kwani atakuwa tayari kucheza, hivyo kuna uwezekano wa kuwepo kwenye mchezo wetu ujao dhidi ya Mbao.

“Ameshindwa kucheza dhidi ya Toto kwa sababu tuliona tumpumzishe kwa kuwa kidonda kilikuwa bado kibichi na uvimbe ulikuwa mkubwa kiasi cha kumfanya kutokauka haraka, alitakiwa kukaa mpaka kipone kabisa kama ilivyo sasa ndiyo atolewe na aweze kuungana na wenzake,” alisema Bavu.


Stori zinazo husiana na ulizosoma

Toa comment