Daktari Mhindi Anayedaiwa Kumfanyia Mbongo Upasuaji Kimagumashi Kimenuka

KIMEWAKA! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kucharuka na kumtaka daktari wa Kihindi, Annapurna Dama kufika mahakamani hapo kujibu tuhuma zinazomkabili za kudaiwa kumfanyia upasuaji wa kimagumashi Aziza Salumu. 

 

Aziza (pichani) katika kesi hiyo ya madai namba 3 ya mwaka 2017 anadai kwamba Dk. Dama alimfanyia upasuaji wa utumbo mkubwa badala ya upasuaji wa kuondoa matatizo kwenye vifuko vya mayai (Fibroids) yaliyokuwa yakimfanya augue.

 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania tayari amemuandikia hati ya kuitwa shaurini daktari Dama Juni 14, mwaka huu ikimuamuru kufika bila kukosa mbele ya Jaji Atuganile Florida Ngwala, yeye au wakili wake anayeruhusiwa kisheria Julai 25, mwaka huu saa tatu asubuhi.

 

“Unaagizwa kuleta vielelezo vyote ambavyo unatarajia kuvitumia kwa ajili ya utetezi siku hiyo,” imesema sehemu ya nyaraka hiyo ya mahakama ya kuitwa shaurini.

 

Aidha, Dk Dama amepewa angalizo na Mahakama Kuu ya Tanzania kwamba kama siku hiyo hatafika na mahakama ikajiridhisha kwamba ana taarifa ya wito huo, kesi itasikilizwa upande mmoja na kutolewa maamuzi bila yeye (Dk Dama) kuwepo mahakamani.

 

Kesi hiyo inasimamiwa na Wakili Richard Mmbando ambaye katika nyaraka zake amesema, Aziza anastahili kulipwa shilingi milioni 400 na daktari huyo ambaye alikuja hapa nchini kwa kikazi pamoja na chombo alichokuwa akifanyia kazi (kwa maana ya hospitali mmoja iliyopo jijini Dar ambayo jina lake linahifadhiwa kwa sababu maalum) kwa madai kwamba uzembe huo amemsababishia matatizo mazito ya kiafya mteja wake.

 

Nyaraka hiyo ambayo imewasilishwa Mahakama Kuu ya Tanzania kama moja ya kielelezo inasema kwamba Aziza alilazwa na kutibiwa na daktari huyo Januari 21, mwaka 2015 baada ya kupewa miadi ya kuonana naye kwa kadi yenye namba 26-15-18.

 

Wakili Mmbando amesema mteja wake alifanyiwa uchunguzi mbalimbali na kuonekana kwamba ana matatizo katika via vya uzazi hususan kwenye sehemu ya kutengeneza mayai (Fibroids) hivyo kupangiwa kufanyiwa upasuaji kuondoa tatizo hilo Januari 22, mwaka 2015.

 

“Hivyo basi Januari 22, mwaka 2015 mteja wangu alifanyiwa upasuaji kwenye utumbo mkubwa badala ya kwenye mirija ya mayai (Fibroids) na akapewa ruhusa kurudi nyumbani Januari 29, mwaka 2015,” imesema sehemu ya kielelezo hicho namba DA -2 (annexture DA-2) kilichopo mahakamani.

Hata hivyo, wakili huyo anadai kwamba Januari 30, mwaka 2015 hali ya mteja wake ikawa mbaya zaidi na akarudi kwa daktari huyo ambapo Januari 31, mwaka huohuo ikabidi apewe rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

 

Wakili huyo amemtaka Dk. Dama kumlipa mteja wake shilingi milioni 400, kama fidia kwa matatizo ambayo amedai ameyasababisha daktari huyo ikiwa ni pamoja na gharama za matibabu ambayo amekuwa akiziingia mteja wake tangu tatizo hilo litokee. Hata hivyo, haikufahamika kama daktari Dama bado yuko chini akiendelea na kazi katika hospitali hiyo au amesharudi kwao India.

 

Wakili Mmbando amepewa kazi ya kumsimamia Aziza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) baada ya mlalamikaji kuomba msaada huo kwa barua ya maombi namba 68 ya mwaka 2016 na mahakama kutaarifiwa kupitia kwa Msajili wa Mahakama Kuu kwa barua yenye kumbukumbu namba TLS/ LAU/ Okt.2016 ya Oktoba 25, 2016.

 

Akielezea hali ya mteja wake katika kielelezo alichoambatanisha mahakamani, Wakili Mmbando amedai mteja wake baada ya kufanyiwa upasuaji huo usiofaa, amepata ulemavu wa kiafya na amekuwa akihangaika kuweka sawa hali yake, vinginevyo angefanyiwa upasuaji kwa makini hivi sasa angekuwa anaendelea na shughuli zake za maisha kama kawaida.

 

Ameongeza kwamba, kufanyiwa upasuaji wa utumbo mkubwa halikuwa tatizo la mteja wake na hali hiyo imemsababishia asijishughulishe na shughuli zake hivyo kumkosesha kipato kiuchumi. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Ngwala, Julai 25, mwaka huu.

Loading...

Toa comment