The House of Favourite Newspapers

Daladala za Sabasaba Dodoma Zagoma

0

MADEREVA na wamiliki wa Daladala, stendi ya Sabasaba jijini Dodoma, wamegoma kutoa huduma ya usafirishaji kwa madai eneo ni dogo, miundombinu mibovu licha ya kutoa ushuru ndani ya halmashauri. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma.

 

Mgomo huo umefanyika leo Jumatano tarehe 13 Januari 2021, kutokana na hali ya stendi hiyo kuwa mbovu hususani wakati wa kipindi hiki cha mvua huku wakidai wanatoa ushuru mkubwa kwa gari kila siku.

 

Mmoja wa madereva na mmiliki wa daladala, Abdul Mohammed amesema, wameamua kusitisha huduma ya usafirishaji ndani ya stendi kutokana na miundombinu kuwa mibovu jambo ambalo halipatiwi ufumbuzi kwa muda mrefu sasa.

 

Mbali na hilo, amesema, mpaka sasa haieleweki kama sabasaba ni stendi au soko kutokana na sintofahamu kwani kuna mchanganyiko ndani ya sitendi hiyo.

 

“Hapa hatujui kama hii ni stendi au soko, tunachotakiwa kujua ni kuwekwa wazi kama stendi hawa wanaouza biashara chini watupishe kama ni soko basi sisi wa daladala tuondoke na tuoneshwe mahali ambapo itakuwa stendi,” amesema Mohamed.

 

“Hapa sabasaba hatujawahi kuhakikishiwa kama ni stendi au ni soko, lakini tunatozwa ushuru wa Sh.1,000 kwa kila gari, zipo gari zaidi ya 3,000 ukifanya Sh.3000×1000 ni sawa na milioni tatu kwa siku ukizidisha kwa mwezi sawa na milioni 9,” amesema.

 

“Lakini wanashindwa kututengenezea miundombini hapa unaona matope yamejaa lakini nagari yanavunja springi, tunashindwa kugeuza tunavunjiana taa za magari lakini mbaya zaidi, tunajikuta tunalipa nyanya au mikokoteni ya wafanyabiashara ndani ya stendi.

 

“Hii tunayoambiwa stendi wamejaa wafanyabiashara ya matunda, mbogamboga, wachoma mishikaki, wauza samaki na wanazuia hata sehemu ya kuegesha.”

 

“Sisi tupo tayari kuhamia popote ambapo uongozi wa Jiji utatupangia kwa kuboresha miundombinu na kama watataka tukae hapa sabasaba basi hawa wafanyabiashara watupishe na miundombinu iboreshwe sambamba na kuweka taa ili kuondokana na vibaka ambao wapo stendi kutokana na kukosekana kwa mwanga”amesema Mohammed.

 

Alipotafutwa mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ili aweze kuzungumzia malalamiko hayo hakuwa tayari na aliingia katika gari yake na kuondoka.

Leave A Reply