Agosti 12, 2004
Posta, Dar es Salaam.
Kishindo kikubwa na kizito kilisikika eneo lote na kusababisha mpaka majengo yatingishike utafikiri kumetokea tetemeko la ardhi, watu waliokuwa wakiendelea na shughuli zao za kawaida, waliacha kila kitu na kuanza kukimbilia mahali kishindo hicho kilikotokea, kila mtu akiwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia ni nini hasa kimetokea.
“Ameua! Ameua!”
“Kwani kumetokea nini?”
“Hata sijui, twende tukashuhudie,” alisema mwanaume mmoja huku akiongeza mwendo, yule aliyemuuliza naye akaongeza mwendo na kuungana na watu wengine wengi waliokuwa wakielekea eneo la tukio.
“Mungu wangu!” alisikika shuhuda mwingine, akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona mbele ya macho yake. Gari kubwa la mchanga, lililokuwa na maandishi makubwa ubavuni, Stutgart Ginstar Gravel and Aggregates, lililokuwa likipeleka mchanga kwenye ghorofa kubwa lililokuwa likijengwa katikati ya Jiji la Dar es Salaam, eneo la Posta lilikuwa limelivaa basi dogo lenye rangi ya njano, lililokuwa likitumiwa na wanafunzi wa shule ya msingi inayotumia mchepuo wa Kiingereza (English Medium), Tanzanation International School.
Hali ilikuwa ya kutisha kwenye eneo la tukio, viatu vya watoto wadogo, mabegi na madaftari yalikuwa yametapakaa eneo lote, huku damu nyingi zikionekana pia. Ilikuwa ni ajali ambayo iliwashtua mno watu wote walioshuhudia kilichotokea.
“Mungu wangu! Ina maana huyu dereva wa lori alikuwa haoni kama kuna gari jingine wakati anakata kona na kuingia kwa kasi kubwa?” alisikika shuhuda mwingine aliyekuwa akizungumza eneo la tukio, hakuna aliyekuwa na majibu.
Ilibidi zoezi la uokoaji lianze haraka sana, basi hilo dogo ambalo lilikuwa limepinduka na kuyafanya magurudumu yake yawe juu, huku yakiendelea kuzunguka, lilikuwa limenasa kwenye mtaro, mahali liliporushwa baada ya kugongwa ubavuni na lori hilo kubwa ambalo dereva wake alifanikiwa kutoroka katika mazingira ambayo hakuna aliyemshtukia.
“Haya ndiyo matatizo ya madereva wanaofanya kazi wakiwa wamelewa viroba, huu ni uzembe wa hali ya juu, angalia anapoteza roho za malaika hawa,” alisikika mwingine, kila mmoja akawa anaunga mkono kwamba ajali hiyo ilikuwa imesababishwa na uzembe wa waziwazi wa dereva wa lori hilo.
“Jamani lawama hazisaidii kwa sasa, hebu tuwasaidieni hawa watoto,” alisema mwingine, kazi ya kufungua mlango wa basi hilo dogo ikaanza. Haikuwa rahisi kwa sababu upande kulipokuwa na mlango, ndipo kulipogongwa na kubonyea vibaya. Baada ya kazi kubwa, iliyoongozwa na mafundi waliokuwa wakichomelea mageti kwenye jengo lililokuwa likiendelea kujengwa, hatimaye kipande cha mlango kilikatwa na kutolewa, kazi ya kuanza kuwatoa watoto wadogo waliokuwa wamejeruhiwa vibaya, ikaanza.
“Maskini malaika wa Mungu, wala hawana hatia yoyote,” alisikika mwanamke mwingine ambaye alishindwa kujizuia na kuanza kuangua kilio, hasa baada ya kuona jinsi watoto hao walivyokuwa wamejeruhiwa vibaya.
Ilibidi wasamaria wema watoe magari yao kusaidia kuwakimbiza hospitali watoto hao ambao idadi yao ilikuwa kati ya ishirini hadi thelathini, pamoja na mwalimu wao mmoja na dereva. Honi za magari yaliyokuwa yakikimbia kuelekea Hospitali ya Muhimbili zikaanza kusikika huku wasamaria wema pia wakijitahidi kuwaelekeza madereva wengine kuyapisha magari hayo.
Muda mfupi baadaye, gari la kubebea wagonjwa pia lilifika, sambamba na askari wa usalama barabarani ambao walianza kuchunguza chanzo cha ajali hiyo muda huohuo, huku dereva wa lori akianza kusakwa kwa udi na uvumba. Ilibidi barabara hiyo ifungwe kwa muda, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wengine wa barabara.
“Mh! Sijui kama watapona maskini ya Mungu, wengi wamejeruhiwa vibaya sana, eeh Mungu onesha miujiza yako,” alisikika muuza magazeti mmoja wa eneo hilo, ambaye mikono yake ilikuwa imelowa damu, baada ya kushiriki kikamilifu kuwasaidia majeruhi wa ajali hiyo ya kutisha.
Gumzo liliendelea kuwa kubwa, habari zikasambaa kwa kasi kubwa kona zote za Jiji la Dar es Salaam, wazazi ambao watoto wao walienda shule asubuhi hiyo wakawa wanahaha huku na kule.
***
“Haloo!”
“Haloo!”
“Samahani, wewe ni mzazi wa Wahida?”
“Ndiyo, nani mwenzangu?”
“Mimi ni mwalimu wake, nasikitika kukutaarifu kwamba gari la shule lililokuwa limewabeba wanafunzi limepata ajali eneo la Posta sasa hivi na hivi tunavyozungumza, mwanao na watoto wengine wanakimbizwa Hospitali ya Muhimbili, fika haraka hospitalini,” alisikika mwalimu kisha simu ikakatwa.
Zilikuwa ni taarifa zilizomshtua mno Denilson, mwanaume wa makamo aliyekuwa mwajiriwa wa benki kubwa ya Dixim Finance iliyokuwa Kariakoo, kitovu cha biashara cha Jiji la Dar es Salaam. Ni muda mfupi tu uliopita, alikuwa na mwanaye huyo wa kipekee, Wahida, akaagana naye wakati akienda kazini na kumuacha nje ya nyumba yao akiwa na msichana wa kazi, wakisubiri basi la shule, mkewe akiwa bado amelala. Alilikumbuka vizuri hata tabasamu lake alilolitoa wakati akiagana naye.
“Bye baba!”
“Bye mwanangu!”
“Jioni uniletee zawadi.”
“Usijali mwanangu, nitakuletea. Na wewe ukawe makini na masomo shuleni.”
“Sawa baba, nakupenda!”
Alikumbuka jinsi alivyoagana naye, picha yake ikajaa akilini mwake na kumfanya apoteze kabisa utulivu, akaacha kila alichokuwa anakifanya na kusimama.
“Vipi, uko sawa?”
“Hapana, nimepokea taarifa ambazo kidogo siyo nzuri.”
“Nini tena?”
“Gari la shule lililokuwa limebeba wanafunzi, akiwemo mwanangu Wahida limepata ajali, inatakiwa niende Muhimbili sasa hivi,” alimwambia Jason, mfanyakazi mwenzake ambaye kabla ya simu hiyo kupigwa, walikuwa kwenye mazungumzo ya kikazi ambayo ghafla yalikatika.
Kila kitu kilikuwa kimetokea kwa kasi kubwa sana, ndani ya muda mfupi tayari Denilson alikuwa ndani ya gari lake akikimbia kwa kasi kuelekea hospitalini. Alijihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wake kwa sababu mara nyingi, hakuwa akiruhusu mwanaye apande basi la shule, alikuwa akimpeleka mwenyewe mpaka shuleni kisha ndiyo aendelee na shughuli zake lakini ubize wa kazi uliomkabili kwa siku kadhaa, ulimfanya aache utaratibu wake huo. Akiwa anaendelea kuendesha gari kwa kasi kubwa, alimpigia simu mke wake na kumuuliza mahali alipokuwa.
“Kwani wewe umeniacha wapi?”
“Hujajibu swali mke wangu.”
“Bwana eeh, si umeniacha nyumbani? Au wewe unafikiri niko wapi?” alinijibu kwa jeuri kama ilivyo kawaida yake, akajikuta akikata simu bila hata kumpa taarifa ya alichotaka kumwambia.
Miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yakimsononesha sana moyoni mwake na kumfanya muda wote akose raha kiasi cha ufanisi wake kazini kushuka, ilikuwa ni tabia za mke wake alizoanza kuzionesha muda mfupi baada ya kufunga naye ndoa.
Majibu ya hovyo, dharau, kiburi na matusi havikuwa vitu vya ajabu kwake anapozungumza naye, ni kama ilishakuwa sehemu ya maisha yao, hakuwa akimheshimu hata kidogo. Wakati mwingine alikuwa akimtoa nishai hata mbele ya rafiki zake au wafanyakazi wenzake, achilia mbali mtoto wao wa kipekee, Wahida.
“Mtoto amepata ajali yuko Muhimbili,” aliamua kumtumia meseji akiwa njiani, muda mfupi baadaye akapiga, safari hii akiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea. Denilson alimjibu kwa kifupi kwamba na yeye amepigiwa simu na kwa muda huo alikuwa njiani akielekea hospitali.
Muda mfupi baadaye, tayari alishawasili Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akashuka mbiombio hadi eneo la ‘emergency’ ambako aliwakuta wanafunzi wengine wakiwa wanaendelea kupokelewa, kutoka kwenye magari binafsi na ambulance na kupakizwa kwenye vitanda vya magurudumu na kuingizwa wodini.
Denilson aliangaza macho huku na kule, hofu kubwa ikiwa imetanda ndani ya moyo wake.
“Aroo, huruhusiwi kusogea huku, simama kule,” mlinzi aliyekuwa na kirungu mkononi alimwambia Denilson kwa ukali, akaona ni kama anamchanganya kichwa tu, akampuuza na kuvuka kwenye kamba maalum iliyokuwa imewekwa eneo hilo, akasogea mpaka pale watoto walipokuwa wakiendelea kushushwa.
“Aroo wewe! Si naongea na wewe?”
“Aisee hebu niache basi, mwanangu amepata ajali na sijui yupo kwenye hali gani, kwani huna shughuli nyingine za kufanya?” alimjibu kwa ukali.
“Sawa, pamoja na yote lazima ufuate utaratibu, unafikiri kila mzazi akijaa hapa manesi watafanyaje kazi yao? Nakuomba uondoke,” alisema huku safari hii akitaka kumshika mkono.
Alitamani kumvaa lakini akaona ataongeza matatizo yasiyo ya lazima, akasogea na kusimama pembeni, mahali ambako wazazi wengine pia walikuwa wamesimama, wengine wakilia na wengine nyuso zao zikiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea pamoja na hali za watoto wao.
Aliendelea kuangaza macho huku na kule, akiwa amekosa kabisa utulivu lakini hakumuona Wahida, hofu ikazidi kutanda ndani ya moyo wake. Mpaka mtoto wa mwisho anatolewa kwenye ambulance na kuingizwa ndani, Wahida hakuwepo.
Akahisi huenda alikuwa miongoni mwa majeruhi wa mwanzomwanzo kufika hospitalini hapo, ikabidi aingie ndani kwenda kuulizia. Kila aliyemuuliza hakuwa anampa ushirikiano, manesi nao wakawa wakali kama mbogo wakiwaambia kwamba walimu wa wanafunzi hao ndiyo pekee waliokuwa wakiruhusiwa kuingia ndani. Muda mfupi baadaye akamuona mke wake naye akiwasili hospitalini hapo, lakini hakuwa peke yake, kuna mtu alikuwa ameongozana naye.
“Imelda! Imelda!” alimuita mkewe huyo ambaye japokuwa aligeuka na kumtazama, hakumjibu chochote, akampuuza na kwenda mpaka kwa nesi aliyekuwa eneo hilo, akawa anazungumza naye huku yule mtu aliyekuja naye akiwa amesimama nyuma yake.
Kwa ilivyoonesha, Imelda na mtu huyo walikuwa wakifahamiana vizuri na pia walikuwa wamezoeana sana maana hata walivyokuwa wamesimama, walisogeleana sana. Baada ya kuzungumza kidogo na yule nesi, Imelda alitoa kitambaa kwenye pochi yake kubwa, akashusha miwani yake na kujifuta machozi kisha akaivaa tena.
Akageuka na kumtazama Denilson ambaye bado alikuwa ameganda kama amepigwa na shoti ya umeme, akishangaa kwa nini mkewe amfanyie vile, tena mbele za watu katika kipindi ambacho alikuwa kwenye wakati mgumu mno.
Ni kweli alishazoea kutolewa nishai na mkewe lakini hakutegemea kama anaweza kuvuka mipaka na kumuoneshea dharau ile pale hospitalini. Alimtazama kwa sekunde chache, uso wake ukiwa umejaa dharau za hali ya juu, akageuka na kuondoka, yule mtu akimfuata nyuma, Denilson akabaki ameduwaa.
Alimtazama yule nesi aliyezungumza na mkewe, akamuona akiandika kitu kwenye daftari, mkono mmoja akiwa ameshika bahasha ya khaki aliyokuwa akihangaika kuificha isionekane. Denilson hakuelewa kama bahasha hiyo alipewa na mkewe au alikuwa nayo kabla lakini akashtushwa na jinsi alivyokosa utulivu.
Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia hadithi hii mpya Jumanne ijayo kwenye Gazeti la Uwazi.
Comments are closed.