Darleen Avunja Ukimya Ugomvi Na Mke Mwezake!

First Lady wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’, amevunja ukimya juu ya tuhuma za kuwa na ugomvi na mke mwenzake, Sabra kwenye mitandao ya kijamii na kuonekana kuna tatizo kubwa.

 

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA, Queen Darleen alisema kuwa, hajawahi kurusha vijembe kwenye mitandao ya kijamii kwa mke mwenzake kwa sababu ni mwanamke ambaye anamheshimu mno.

Mwanamama huyo anasema kuwa, alimkuta kwenye ndoa na ni mke wa kwanza, hivyo hawezi kumpiga vijembe kama inavyoenezwa mitandaoni.

 

“Siwezi hata siku moja kumpiga vijembe yule dada, ninamheshimu mno.“Kwanza amenikosea nini? Mimi nimemkuta na ni mke mkubwa, lazima nimpe heshima yake,” anasema Darleen.

Akiendelea kuzungumza na gazeti hili, Darleen alisema kuwa, watu wakimuona anarusha vijembe, labda amekwazana na mtu mwingine tofauti ila siyo Sabra kwa sababu hafikirii kumfanyia chochote kibaya kwenye maisha yake.

 

“Unajua kuna wakati watu wanashindwa kuelewa labda kuna mtu mwingine amenikwaza wa tofauti kabisa, ukiweka tu jambo lako kwenye akaunti yako, wanaanza kuchamba kwamba ninamsema mke mwenzangu. Jamani mimi siyo wa hivyo hata kidogo na wala sina uswahili huo.

 

“Yule ni mwanamke kama mimi, kwa nini nimfanyie visa?” anasema Queen Darleen anayesemekana tayari amenasa mimba ya mumewe huyo, Isihaka Mtoro aliyefunga naye ndoa miezi kadhaa iliyopita.

 

Tangu Queen Darleen aolewe kama mke wa pili na jamaa huyo ambaye ni mfanyabiashara maarufu jijini Dar, kumekuwa na maneno mengi kuwa hana uhusiano mzuri na mke mwenzake huyo.

Stori: Imelda Mtema, Ijumaa

Toa comment