Davido Aomba Pesa Kimasihara kwa Mashabiki, Apewa Tsh Mil 715
MWANAMUZIKI kutoka nchini Nigeria David Adeleke Adeleji maarufu Davido ameibua gumzo mitandaoni baada ya kutangaza kuanzisha kampeni ya kuwaomba mashabiki pamoja na watu wake wa karibu mchango kwa ajili ya maandalizi ya siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake (Birthday).
Kinyume na fikra za wengi kuwa kampeni hiyo kuwa inaweza isifikie malengo kulingana na kukosa mashiko, Kama utani msanii huyo ameendelea kuingiza pesa nyingi kutoka kwa mashabiki pamoja na watu wake wa karibu wakiwamo wasanii wenzake kutoka mataifa mbalimbali.
Davido ameanzisha challenge hiyo siku ya Novemba 17, 2021. akiwaomba watu kumchangia pesa kwa ajili ya siku yake ya Kuzaliwa ambayo ni Novemba 21 mwezi huu wa 11.
Kabla ya kutangaza rasmi uhitaji wa mchango huo, Davido alifungua akaunti maalum kwa ajili ya kupokea pesa hizo ambapo akiwa LIVE kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram aliwataja wasanii kadhaa akiwa Diamond Platnumz toka Tanzania akiwataka wamchangie.
Na baada ya takribani dakika thelathini pekee tangu kutangaza rasmi challenge, Davido alionyesha kuwa tayari amefanikiwa kukusanya kiasi cha pesa kisichopungua (Naira 128M) ambazo ni sawa na Sh 715 milioni.