DAZ BABA AFUNGUKA CHANGAMOTO ZA MAISHA ZILIVYOMPOTEZA

DAZ Baba ni miongoni mwa majina yaliyotikisa kwenye gemu la Muziki wa Bongo Fleva mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Jina hili ni la mshikaji ambaye alikimbiza kimuziki akiwa ndani ya Kundi la Daz Nundaz, lakini mbali na kundi hilo hata alipokuwa akisimama peke yake alikuwa anafanya vizuri pia.
Miongoni mwa kazi zake ambazo alifanya kwenye gemu la Bongo Fleva na hazitasahaulika kwa mashabiki wa muziki wa enzi hizo ni Elimu Dunia. Na hapa Risasi Mchanganyiko linakukumbusha mistari michache kutoka kwenye wimbo huo;
“Fikra za ajabu, kiburi pamoja na zogo, nilionekana ninazo tangu nikiwa mdogo, michezo ya hatari pamoja na dhuluma, kiburi kwa wakubwa zangu waliponituma, ndipo wazazi wangu walikaa chini wakafikiri, japo kuwa mimi mkubwa nianze skuli, ndipo nilipoanza la kwanza mpaka la pili, ambapo kamali na jeuri vikashamili;”

Bila shaka kutokana na mistari hiyo kuna baadhi ya watu watakuwa wamekumbuka mbali katika matukio fulanifulani au rafiki zao waliyokuwa wakimsikiliza pamoja Daz Baba pengine hawapo pamoja tena.
Hivyo ndivyo maisha yalivyo kwani hata huyo Daz Baba ambaye anaku-kumbusha mbali aliyetamba na nyimbo nyingi ukiwemo huo Wimbo wa Elimu Dunia, Namba Nane, Nipe Tano na Wife aliomshirikisha marehemu Albert Mangwea hasikiki tena kwenye gemu. Ufalme wake ushaporwa.
Wengi mnaweza kuwa mnajiuliza yupo wapi? Anafanya nini? Na ana mipango gani ya kimuziki tena kwa sasa? Risasi Mchanganyiko, limekuletea huyu hapa, msikilize katika mahojiano ‘exclussive’ aliyofanya;
Risasi: Daz niaje upo wapi siku hizi mtu mzima?
Daz Baba: Nipo hapahapa mjini.
Risasi: Unafanya ishu gani kwa sasa?
Daz Baba: Nakomaa na muziki, ingawa nina michongo yangu ya hapa na pale katika harakati za maisha ikiwemo kujikita kwenye ishu za utalii.
Risasi: Safi sana, umesema bado unakomaa na muziki lakini husikiki, sasa huo muziki unakomaa nao wapi?
Daz Baba: Sisikiki tu kwa sababu ya changamoto za hapa na pale , lakini nina kazi ipo kwenye mitandao na nipo ninajiandaa kutoa albamu yangu ya tatu baada ya Elimu Dunia na Dunia ya Leo niliyotoa mwaka 2009, hii itaitwa Hali Siyo Hali.
Risasi: Albamu hiyo inatarajiwa kutoka lini, umemshi-rikisha nani na umefanyia studio gani?
Daz Baba: Kila kitu kitakuwa ‘surprise’, lakini mashabiki wangu wakumbuke nimewahi kufanya kazi kwenye studio kubwa zikiwemo Bongo Records, Fish Club na nyingine nyingi. Kwa hiyo hata katika hii albamu wategemee kuona kazi kutoka studio mbalimbali kubwa lakini pia nitafanya kazi na kundi langu la Tanzaniano.

Risasi: Kwenye hili kundi upo na kina nani?
Daz Baba: Jamaa wenye vipaji na wengi wapo nje, watatua Bongo ‘soon’ kwa ajili ya kuungana na mimi na nitawatambulisha rasmi.
Risasi: Lakini nini hasa kilikupoteza kwenye gemu Daz na ‘unamiss’ nini kwenye ‘main stream?’
Daz Baba: Nishazungumza sana, kikubwa ni changamoto za kimaisha na hapa sifikirii kama nitaulizwa kuhusu madawa na nini kwani ni vitu ambavyo siwezi kuzungumzia. Lakini kikubwa kwenye gemu ninamiss kuruka na mashabiki wangu na ninaamini kwa namna nilivyojipanga nitarudi na kuendelea kama ilivyokuwa awali.
Risasi: Nikushukuru sana Daz Baba, kama una lolote karibu.
Daz Baba: Kikubwa mashabiki wangu wategemee makubwa kutoka kwangu kwani nimejipanga vizuri na ninategemea kurudi kwa kasi nyingine.
MAKALA: Boniphace Ngumije


Comments are closed.