The House of Favourite Newspapers
gunners X

DC Magoti Azindua Taasisi ya Planet Servers Iliyojipanga Kulinda Mazingira

Mkurugenzi wa Planet Servers Foundation, Tatu Zuberi Tumbi akizungumza na wanahabari (hawapo pichani).

Pwani, 14 Februari 2025: Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti amezindua taasisi isiyo ya kiserikali ya Planet Servers Foundation yenye Makao yake Makuu Kisarawe yenye lengo la kutunza mazingira, usafi na kulinda uoto wa asili kwa kupanda miti sehemu mbalimbali ikianzia na maeneo ya huduma za kijamii kama vile shuleni na kwingineko na kutoa elimu ya mazingira na shamba darasa.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti.

DC Magoti aliipongeza Planet Servers Foundation iliyokuja na mkakati huo ambao utakwenda kulinda na kuokoa mazingira na hivyo kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan za kulinda mazingira.

Akizungumza na wanahabari baada ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Tatu Zuberi Tumbi amesema ameelezea jinsi taasisi hiyo jinsi itakavyofanyakazi hizo na kutoa elimu kwa jamii na kuendelea kusema;

“Naamini taasisi hii itakuwa mkombozi wa mazingira hapa Kisarawe na hatimaye kwingineko, mimi ni mdau mkubwa wa mazingira na nilianza harakati hizi muda mrefu tangu nikiwa Arusha nilikuwa nikiwashirikisha kinamama wenzangu kupanda miti pembezoni mwa barabara ya East Africa.

“Wakati tukifanya hayo lengo langu kubwa lilikuwa ni siku moja Mungu anijaalie  kufungua taasisi hivyo leo ndoto yangu imetimia.

“Hivi tunavyoongea zoezi hili tumeshalianzia hapahapa Kisarawe tukianzia na kupanda miti kutoka ‘keep lefti’ cha Kisarawe mjini barabara yote kuelekea mpaka ofisi ya mkuu wa wilaya, tumeshapanda miti ya kimvuli na ya matunda.

“Pia tumepanda miti kwenye shule moja iitwayo Vibura na Februari 15 mwaka huu (kesho) tunaenda kupanda miti kwenye shule nyingine.

Lengo letu kubwa ni kupanda miti mashuleni na kutoa elimu ya kutunza mazingira tukianzia ndani ya Kisarawe kisha kwingineko na hatimaye nchi nzima.

“Tumedhamiria kufanya hayo kutokana sehemu mbalimbali mazingira kuharibiwa kama vile kwenye vyanzo vya maji na ukataji wa miti hovyo.

Pia tunafanya haya katika kumuunga mkono, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mdau mkubwa wa kutunza mazingira. HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN /GPL

Comments are closed.