The House of Favourite Newspapers

DC Temeke na Mbunge Kilave Wawafunda Bodaboda Kuiheshimu Kazi Yao

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda akiijaribu moja ya pikipiki zilizokuwa zikizinduliwa.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo Dorothy Kilave wamewaasa maafisa usafirishaji kwa njia ya pikipiki maarufu kama maafisa usafirishaji kuifanya kazi hiyo kwa nidhamu kwani ni kazi yenye thamani kama kazi zingine.
DC Mapunda ameelezea kukerwa kwake na bodaboda wenye tabia ya kuendesha bodaboda huku wakiwa wamejipinda makusudi huku wakining’iniza kandambili au wengine wakijipinda kama wanasikilizia sauti ya pikipiki kutokea kwenye bomba la moshi na kutovaa kofia ngumu (helmet) na kuvunja sheria za barabarani kusema hizo ni tabia ambazo wanazomkera waendesha bodaboda.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mh. Sixtus Mapunda (wa pili kushoto) akijaribisha moja ya piki piki wakati wa uzinduzi wa pikipiki mpya za Daima na Everlast katika viwanja vya TCC Club- Gwambina Jijini Dares Salaam. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Alternative Solution Limited, Ruge Chacha, Mbunge wa Temeke Dorothy Kilave na Diwani wa Viti Maalumu Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Caroline Hendrich.
DC Mapunda amesema hayo wakati akizindua pikipiki mpya aina ya Daima na Everlast,  katika viwanja vya TCC Club Chang’ombe, Jijini Dar es Salaam, ambapo alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh. Albert Chalamila.
DC Mapunda, aliipongeza kampuni ya Alternative Solution Limited, ambao ndio wasambazaji wa pikipiki hizo kwa uthubutu wao na kuwaletea watanzania bidhaa bora.
“Inapendeza kabisa kuona sisi watanzania wenyewe tukitafuta suluhisho ili kuleta unafuu katika sekta hii ya usafirishaji kwani pikipiki zinatumika kila mahali nchini na zinarahisisha usafiri wa abiria na mizigo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine,” alisema.
Alitoa wito kwa watumiaji wa pikipiki  hususani bodaboda kufuata sheria za barabarani na kuzingatia matumizi sahihi ya pikipiki kama wanavyoshauri wataalamu ili zidumu kwa muda mrefu. “Tunao wataalamu hapa leo naomba tuwasikilize ili matumizi yawe bora na pamoja na mambo mengine tupunguze ajali,” alisema.
Alitoa wito kwa mashirika mbalimbali ya kifedha yaingie makubaliano na Alternative Solution Limited ili kuhakikisha waendesha boba boda wengi wanajengewa uwezo wa kumiliki pikipiki zao wenyewe kwa utaratibu mzuri usiowaumiza.
Kwa mujibu wa Mh. Chalamila tayari Jiji la Dar es Salaam limeanza kufanya kazi saa 24 na moja ya usafiri unaotegemewa na watu wengi ni pikipiki. “Uzinduzi huu umekuja muda mwafaka wakati bidhaa hii inahitajika,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Alternative Solution Limited, Bw. Ruge Chacha alisema kampuni hiyo ilifanya utafiti wa kina ili kujua mahitaji ya watanzania hususani watumia pikipiki na changamoto wanazopitia kabla ya kuziagiza.
Alisema pikipiki za Daima na Everlast zina faida nyingi zaidi ikilinganishwa na pikipiki nyingine ikiwemo kuwa na nafasi kubwa ya kukalia kwa dereva pamoja na  abiria lakini pia pa kubebea mizigo, sehemu ya kuhifadhi na kuchajia simu, sehemu ya kuwekea chupa ya maji upande wa kulia na taa imara inayoona vizuri hata wakati wa mvua na giza.
Bw Chacha alibainisha kuwa piki piki hizo zina zina matairi imara kabisa yanayowezesha kupakia abiria na mzigo mzito bila wasiwasi yoyote kwani kuna sehemu maalumu ya mizigo ambayo pikipiki nyingine hazina kabisa.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau zaidi ya 300 wa sekta ya usafirishaji hususan pikipiki na baadhi walipata fursa ya kujaribisha na kuuliza maswali kuhusu pikipiki hizo mpya.
Naye Mbunge wa Jimbo la Temeke, Mh. Dorothy Kilave aliahidi kuendelea kushirikiana na waendesha boda boda wote Kwa kuzingatia umuhimu wao katika jamii.
“Zingatieni Sheria za barabarani na mnunue pikipiki za Daima na Everlast zitawasaidia,” alisema.
Baada ya uzinduzi huo piki piki hizo za Daima na Everlast zitasambazwa nchi nzima kupitia mawakala tofauti tofauti.