DED Malinyi Apata Ajali

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi (DED), Mkoa wa Morogoro, Joanfaith Kataraiya na dereva wake wamejeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea jana Jumapili baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kupasuka tairi ya mbele ya kushoto na kupinduka kijiji cha Usangule wilayani humo.

 

Joanfaith alikimbizwa katika Kituo cha Afya Mtimbira na sasa anaendelea kupatiwa matibabu hospitali ya Mtakatifu Francisco Mjini Ifakara.

 

Kwa mujibu wa mbunge wa jimbo hilo, Antipas Mgungusi amesema alikuwa akitokea Morogoro Mjini kwenye majukumu yake ya kazi akirejea kwenye eneo lake la kazi.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Mathayo Masele alisema ajali hiyo ilimetokea Septemba 05, mwaka huu saa moja kasoro jioni na kwamba walipata taarifa ya ajali hiyo majira ya jioni kutoka kwa mkurugenzi mwenyewe baada ya kunusurika na walifika eneo la ajali kijiji cha Usangule kilometa 25 kabla ya kufika Malinyi.

 

Amesema licha ya maendeleo mazuri ya mkurugenzi huyo aliyejeruhiwa zaidi miguuni na dereva aliyelalamikia kuumia mgongo na kichwa, ajali hiyo ilikuwa ni mbaya kwa tairi kupasuka na gari kupinduka na tairi kuwa juu.

“Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ilifika kwa wakati eneo la tukio na kutoa msaada wa dharura kuwanusuru mkurugenzi na dereva wake ambapo majira ya saa moja na nusu usiku tuliwakimbiza kituo cha afya cha Mtimbira kwa matibabu ya awali na kuweka mazingira mazuri eneo la ajali ili isisababishe ajali nyingine,” alisema mkuu huyo.

 

Hata hivyo alisema majeruhi hao wawili waihamishwa kutoka kituo cha afya Mtimbira majira ya saa tano usiku baada ya matibabu ya awali na kupelekwa hospitali ya Rufaa ya St Francis iliyopo Ifakara wilayani Kilombero kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kiafya na matibabu zaidi.

 

Kuhusu alikokuwa akitokea na kuelekea mkurugenzi huyo, DC Masele alisema alikuwa eneo lake la kawaida la kazi na alikuwa akirejea Malinyi kuendelea na majukumu yake ya kawaida, akitokea mjini Morogoro kwa vikao.

 


Toa comment