The House of Favourite Newspapers

Denti Apewa Mimba na Bab’ake Mzazi

 

HIVI dunia inakwenda wapi? Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mkenyenge wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, (jina linahifadhiwa), amemtaja baba yake mzazi aitwaye Kidumali kuwa amemgeuza mkewe na kumpa ujauzito uliosababisha kufukuzwa shule. 

 

Madai hayo mazito yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Richard Abwao alipozungumza na Uwazi hivi karibuni ambapo alisema binti huyo alimtaja baba yake mwenye miaka 45 kuwa ndiye aliyempa mimba hiyo na sasa taratibu za kisheria zinafuatwa ili afikishwe mahakamani.

 

Awali akizungumza na Uwazi, binti huyo mwenye umri wa miaka 17 alidai kuwa ujauzito wake una miezi saba, ni wa baba yake na kwa sasa anaishi katika Kijiji cha Bulimba.

 

“Ujauzito huu ni wa baba. Niliishi na baba peke yetu, wadogo zangu waliondolewa na baba wakaenda kuishi na bibi yetu baada ya mama kufariki,” alisema mtoto huyo. Alidai kuwa alipopata ujauzito huo alikwenda kumueleza bibi yake lakini alimsihi kutomtaja baba yake kwa kuwa ni aibu kwa familia na kwamba amtaje mfanyabiashara aitwaye Alex.

“Nilipoanza kuugua nilimueleza baba kuhusu hali yangu, alinipeleka kwa mganga wa kienyeji ili niitoe ikashindikana, akawa ananipa muarobaini ninywe ili itoke ikashindikana, mwisho alininunulia koti kubwa niwe nalivaa ili isionekane,” alidai mwanafunzi huyo.

 

Alidai wanafamilia walimuambia kuwa kumtaja baba yake mzazi ni kitendo cha aibu katika ukoo hivyo wakamshauri amtaje jamaa Alex ambaye ni mfanyabiashara.

 

Shangazi wa mtoto huyo, Esther Kidumali alikiri kuwa mwanafunzi huyo alikuwa akiishi na baba yake mzazi baada ya mama yake mzazi kufariki dunia miaka mingi iliyopita lakini akashangazwa na kitendo cha ndugu yake kukamatwa na polisi.

 

“Hivi sasa baba yake hatufahamu kwa nini anashikiliwa na jeshi la polisi. Wanafamilia tulimhoji mwanafunzi huyu kama baba yake anashikiliwa kwa sababu amemtaja, alikataa, akadai alimtaja Alex,” alidai shangazi yake. Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho akiwemo Eliza John walisema walikuwa wakimuona mtoto huyo akiishi na baba yake pekee kwenye nyumba yao ila wakawa hawana uhakika na madai aliyoyatoa.

“Hayo madai aliyoyatoa ni mazito sana dhidi ya baba yake, mimi naomba tu habari hii mbali na kwamba ipo polisi, iwafikie waziri mwenye dhamana ya watoto (Ummy Mwalimu) na yule wa elimu, (Joyce Ndalichako) ili sheria iweze kunyooshwa.

 

“Nasema hivyo kwa sababu, kama ameshaanza kutajwa mtu mwingine ambaye ni huyo Alex sijui, huenda mzigo ukamuangukia mwingine asiyehusika. Kikubwa uchunguzi ufanyike na kama baba ndiye anayehusika na ujauzito huo, sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho maana matukio ya baba kuwatia mimba watoto wao sasa yamekuwa ‘too much’,” alisema Eliza, mama wa watoto wawili.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bulimba kulipotokea mkasa huo, Peter Jibuge amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lakini akasema ameshindwa kutoa msaada wowote kutokana na kauli mbili za mwanafunzi huyo kuhusiana na aliyempa ujauzito.

 

“Awali alimtaja baba yake mzazi kuhusika lakini baadaye alibadili kauli na kumtaja mfanyabiashara aliyedai walikuwa wakikutana gulioni,” alidai kiongozi huyo. Gazeti hili linafuatilia kwa karibu sakata hili ili kujua mwisho wake.

Stori: Mwandishi Wetu, SHINYANGA

Comments are closed.