DENTI CHUO KIKUU ALIYEUAWA KWA VISU UTATA MZITO

KIFO cha mwanafunzi wa Kampala International University (KIU), Anifa Mgaya aliyeuawa kwa kuchomwa kisu Jumapili iliyopita kimeibua utata kufuatia muuaji huyo kushindwa kuchukua vitu vya thamani alivyokuwa navyo marehemu baada ya kutekeleza mauaji hayo.

 

Anifa ameuawa nje ya nyumba aliyokuwa akiishi iliyopo pembezoni mwa chuo hicho wakati akitokea kujisomea majira ya saa mbili usiku.

 

Kufuatia tukio hilo wanahabari wetu walikwenda chuoni hapo na kuonana na viongozi wa chuo hicho ambao waliwaelekeza kumuona Mshana Mshana ambaye ni Mshauri wa wanafunzi wa chuo hicho na muda huo alikuwa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mwanafunzi huyo.

 

Wanahabari wetu walikwenda kwenye nyumba hiyo na kukuta michirizi ya damu iliyotapakaa kutoka barabarani kuelekea kwenye geti la kuingilia ndani na kumkuta Mshana na baba wa marehemu wakivipakia kwenye gari vyombo alivyokuwa akivitumia marehemu.

 

Akizungumza na wanahabari wetu baba wa marehemu alisema anasikitishwa na tukio baya alilofanyiwa mwanaye na kushindwa kuendelea kuzungumza na kubaki akifuta machozi kila alipokuwa akiangalia michirizi ya damu eneo la tukio.“Ninachoweza kusema ni kwamba nasikitika sana kwa tukio alilofanyiwa mwanangu, sina zaidi ya hilo naomba kwa sasa mniache,” alisema baba huyo aliyejitaja kwa jina moja la Mgaya.

Wanahabari wetu walipomuuliza suala la msiba alisema utakuwa Kunduchi Salasala na suala zima la mazishi litapangwa hapo. Baada ya kuzungumza na baba huyo wanahabari wetu walizungumza na rafiki wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Elida Anatory ambaye alikuwa wakiishi nyumba moja alisema;

 

“Anifa aliuawa akiwa anatokea chuoni lakini jambo  linalotushangaza huyo muuaji hakuchukua simu yake wala pochi maana watu wanasema ameuawa na vibaka sasa sijui hao ni vibaka wa aina gani wamuache na vitu vyake vyote vya thamani.

“Wakati akipiga kelele kuomba msaada tulimsikia lakini tulijua huenda ni kelele za mpita njia hatukujua kama ni mwenzetu hivyo hatukuweza kutoka nje haraka kutoa msaada mpaka watu walipoanza kujaa nasi ndiyo tukatoka na kukuta kumbe ni Anifa,” alisema Elida.

 

Mwingine aliyezungumza na wanahabari wetu ni Jafari Uledi ambaye alisema anashangaa mauaji hayo kufanyika majira ya saa mbili usiku muda ambao bado kulikuwa na mishemishe za watu na nguvu kubwa iliyotumika kumdhibiti mtoto wa kike mpaka kumuua.

 

“Kwa ninavyowajua wanawake wengi ni dhaifu kwa wanaume hivyo ukimuonesha kisu tu anakupa chochote alichonacho sasa sijui ilikuwaje mpaka hao wanaosema vibaka watumie nguvu kupita kiasi na kusababisha mauaji hayo kwa binti mdogo kama Anifa, hapo ni lazima kuna jambo,” alisema Uledi.

Faraja James anayesomea madawa (Pharmacy) mwaka wa tatu yeye ameelezea masikitiko yake kutokana na tukio hilo na kusema mwenzao alifariki dunia katika mazingira ya utata sana. “Tunashangaa hao tunaosema vibaka waliomuua mwenzetu kuweza kutekeleza mauaji hayo eneo la wazi kama hili na kutokomea. “Kama ni uhalifu umekubuhu namna hii hadi watu mapema tu wanauawa basi jeshi la polisi liweke kituo eneo hili ili kupunguza uhalifu,” alisema Faraja.

 

Aidha, baadhi ya wanachuo pamoja na majirani walilidokeza Risasi Jumamosi kuwa hawaamini kuwa muuaji ni kibaka bali ni kijana ambaye ametekeleza mauaji hayo kwa sababu zake na hivyo kulitaka jeshi la polisi kulifanyia uchunguzi wa kina tukio hilo baya.

 

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Zuber Chembera alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea.

Waandishi: Richard Bukos na Ezekia Mwanjafu-DSJ

Loading...

Toa comment