Dereva aliyeuawa kwa risasi na Bosi wake, aliyeshuhudia atoboa siri

Marehemu David Kalangula enzi za uhai wake.

Na mwandishi wetu

HAKUNA mauaji ya kikatili yaliyoacha machungu kwa ndugu na wananchi kama ya David Kalangula (36), dereva wa gari la kusafirisha mafuta ya petroli mikoani ambaye anadaiwa kupigwa risasi mbili na bosi wake aliyejulikana kwa jina la Hussein Jatta kwa madai ya kutokea kutoelewana kati yao.

Tukio hilo lililotetemesha nchi na kuacha gumzo kila mahali, lilijiri usiku wa Oktoba 19, mwaka huu maeneo ya Mbagala Mission jijini Dar es Salaam.

ILIKUWA HADHARANI

Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa hadharani na baadhi ya wafanyakazi wenzake wakishuhudia hasa wakati marehemu akipiga kelele kuomba msaada kwa wenzake bila mafanikio.

UWAZI KAMA KAWAIDA YAKE
Uwazi kama ilivyo kawaida yake, baada ya taarifa hizo liliwasili sehemu ya tukio na kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokwepo wakati mauaji yanatekelezwa na mkurugenzi huyo (hawakupenda kutaja majina yao) walikuwa na haya ya kueleza.

Jeneza lililobeba mwili wa marehemu likiombewa.

ILIVYOKUWA

“Tulikuwa bado ofisini, lakini tukiwa tunajiandaa kutoka. Mara, tulisikia mlio wa risasi, mara mbili. Tulipatwa na woga mkubwa. Hata hivyo, tuliamini kuna mfanyakazi atakuwa amepigwa risasi au vyovyote vinginevyo.“Mlio huo wa risasi ulikwenda sambamba na kelele ya mtu akiomba msaada ambaye hatukumjua mara moja ni nani. Ndipo baadaye tuligundua kuwa, ni Kalangula amepigwa shaba kama mnyama,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.

HUYU NAYE ANA LAKE MOYONI

John Mwanyage ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Malori Tanzania lakini pia ni dereva wa kampuni hiyo ambaye alikuwepo eneo la tukio na alifanikiwa kuongea na marehemu muda mfupi kabla ya kupigwa risasi na mazungumzo yao aliyaeleza kama ifuatavyo:

“Nikiwa niko kazini majira ya saa moja usiku, marehemu alifika kwetu na kutukuta. Nilisalimiana naye na kumuuliza kuhusu safari alikotoka, akasema amerudi salama, akaniambia nimuache aegeshe gari kisha akatoe taarifa ofisini.
“Alichukua vielelezo ndani ya gari na kuelekea ofisini kwa mkurugenzi. Kwa bahati mbaya bosi huyo alikuwa nje, naye akawa akienda huko ofisini, hivyo wakafuatana.”

HALI ILIVYOKUWA NDANI YA OFISI

“Ndani ya ofisi kulikuwa na watu wanne. Basi, ghafla tukasikia mlio wa risasi huku marehemu akilia kwa uchungu akisema ananiua…nisaidieni. Kwa vile naijua sauti yake niliamini ni yeye. Nikajiuliza amepatwa na nini? Lakini pamoja na kelele zake za kuomba msaada, hakuna aliyejitokeza kwenda kumsaidia. Haikupita muda tukasikia risasi ya pili, paa! Lakini hatukusikia sauti yake tena!”

BOSI AJITOKEZA, ATAKA MAREHEMU AKIMBIZWE HOSPITALI

“Muda si mrefu, ofisa wa usafirishaji, anaitwa Edwin alitoka ofisini, akawaambia walinzi wamchukue Kalangula na kumkimbiza hospitali. Mkuu wa walinzi yeye aliposikia mlio wa risasi alifunga geti na kuondoka katika eneo la tukio.
“Walinzi waliobakia walipatwa na hasira kufuatia kitendo hicho nao wakakataa kumchukua Kalangula kumpeleka hospitali.

“Walinzi hao walihoji ni kwa nini Kalangula apigwe risasi? Na kama alifanya kosa si bora tajiri huyo angewaambia walinzi wamkamate na kumpeleka polisi kuliko kumpiga risasi?“Hata hivyo, Edwin baada ya kuona hali si nzuri ilibidi ampigie simu meneja mwajiri, Solomon Maugo na kumweleza juu ya tukio hilo ambapo muda si mrefu alifika katika eneo la tukio.”

POLISI WAITWA, TAJIRI HAONEKANI

“Tuliwasiliana na polisi ambao walifika lakini tulipomwangalia Kalangula tuligundua alishafariki dunia. Wakati huo mkurugenzi huyo alikuwa haonekani maeneo hayo. Tulifuatilia kisa cha kupigwa kwake risasi, ikabainika kuwa, kulikuwa na hasara ya lita 70 za mafuta ambapo hata hivyo marehemu alikanusha kuwa hahusiki na upotevu huo na kama wanaona anahusika aliomba aache kazi kuliko kusingiziwa.”

Watoto wa marehemu wakilia kwa simanzi kubwa.

WALIVYOSEMA WENGINE

Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi walisema kuwa, marehemu alikutwa mlangoni katika ofisi ya tajiri huyo huku akiwa amelowa damu, hajiwezi na hilo siyo tukio la kwanza.Walisema Julai mwaka huu, kuna mfanyakazi alimpiga risasi lakini hakufa na akamlipa fedha ili kesi isiende mbele.

GLOBAL INAJUA HIKI

Katika tukio la mfanyakazi mwingine, Gazeti la Risasi Jumamosi la Julai 25, mwaka huu, liliripoti habari ya mfanyakazi mmoja wa kampuni hiyo, Deogratius akidaiwa kupigwa mpaka kung’olewa meno na bosi wake (Jett), kisha kukoswa risasi akidaiwa kumtorosha dereva mwenzake baada ya kupata ajali. Deogratius alitoa malalamiko yake Kituo cha Polisi Chang’ombe Temeke kwa kufungua jalada CHA/RB/5871/2015 SHAMBULIO LA MWILI.

MAREHEMU ALILIPIGIA SIMU UWAZI

Siku ya tukio, jioni ya kuelekea saa moja, marehemu Kalangula alipiga simu ofisi za Gazeti la Uwazi na kuongea na mhariri mmoja ambapo alikuwa akilalamikia vitisho vya bosi wake kwamba alimwambia atamuua kwa vile amesababisha upotevu wa mafuta.

“Jamani hapo najua ni Uwazi. Mimi naitwa David Kalangula, kuna bosi wangu anaitwa Jett, anatishia kuniua. Anasema ataniua kwa sababu nimetia hasara ya mafuta. Mimi ni dereva wa magari ya kupeleka petroli nje ya nchi.
“Unajua mafuta ya petroli unapoyasafirisha, kama kuna joto kali lazima yapungue wakati wa kuyashusha. Nilitoa taarifa kabla ya kushusha kule Zambia nikaambiwa nishushe tu, sasa nashangaa.”

Mhariri alimwambia angeshughulikia malalamiko yake kesho yake asubuhi. Lakini ilipofika asubuhi, habari zilisambaa kwamba, Kalangula aliuawa kwa kupigwa risasi na mtu anayedaiwa ni bosi wake.

MSIBANI KWA KALANGULA

Katika msiba wa Kalangula, nyumbani kwake, Kibamba, Dar wiki iliyopita, waombolezaji wakiwemo wafanyakazi wenzake walikuwa wakilia kwa uchungu huku wakishindwa hata kujieleza.Wafanyakazi hao waliahidi kusimamia kesi hiyo na kutoa ushahidi ili kuhakikisha sheria inachukuwa mkondo wake.

Fikiri Juma aliyekuwa msaidizi wa marehemu wakisafiri pamoja, yeye alikuwa na haya ya kusema:
“Tuliondoka na marehemu Oktoba 3, mwaka huu tukiwa na mzigo wa mafuta wa kuupeleka Zambia. Kila inapofika saa 12 jioni tunatafuta sehemu, tunalala kutokana na utaratibu wa ofisi (kutosafiri usiku).

“Tulipofika Tunduma mpakani tulikaa kwa siku tatu tukisubiri utaratibu katika mizani pia kulikuwa na foleni kubwa ya magari. Tulipofika Kapiri Mposhi (Zambia) katika mizani tuliambiwa mzigo wetu umezidi, tukapigwa faini. Tulipiga simu ofisini wakatutumia fedha.

….Waombolezaji wakilia kwa uchungu.

“Tulipofika mpaka wa Zambia na Kongo, joto lilikuwa juu kiasi kwamba tungeshusha mafuta kungetokea upotevu hivyo tukapiga simu ofisini kuwajulisha kuhusu hali hiyo, wakasema tushushe tu. Tulifanya hivyo lakini kukawa na kiasi cha mafuta kimepotea. Baadaye tuligeuza kurudi Dar.

“Siku ya tukio, kabla ya kufika ofisini (Mbagala), mwenzangu aliniachia gari nisimamie kuoshwa maeneo ya Banda la Mkaa. Yeye akaenda nyumbani kwake kuiona familia. Baada ya kumaliza, nilimpigia simu akaja kulichukua na kuelekea ofisini, mimi nikaenda nyumbani kwangu.”

TAARIFA ZA KIFO

“Baadaye nilishangazwa sana kusikia kwamba eti Kalangula amepigwa risasi na bosi na amefariki dunia. Ilinisikitisha sana ukizingatia kwamba tulisafiri kwa shida tumerudi tukiwa tumechoka, tulitakiwa tupumzike kumbe mwenzangu akapumzishwa kwa risasi.” (machozi).

KAULI YA POLISI

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, ACP Andrew Satta kwa upande wake alikiri Kalangula kuuawa kwa kupigwa risasi na bosi wake akisema ni baada ya marehemu kumshambulia afisa mwajiri.“Malumbano yalianzia kwenye upotevu wa mafuta lita mia tatu ambazo zilipotea akiwa safarini kuelekea Burundi.

“Marehemu alilumbana na afisa mwajiri huyo hadi kufikia hatua ya kusema kama ni hivyo anaacha kazi kitu ambacho mwajiri wake hakukubali na kumwambia kwanza waweke sawa suala la upotevu wa mafuta.

“Kutokana na hali hiyo marehemu alichukia na kuchukua kitu kizito na kumpiga mwajiri. Pembeni alikuwepo mkurugenzi wa kampuni hiyo (Jetta) aliona hali si shwari akachomoa bastola na kumpiga marehemu risasi moja,” alisema kamanda huyo.Hata hivyo, Kamanda Satta alisema tajiri huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi Temeke kwa mahojiano zaidi.

MAREHEMU AZIKWA MBEYA

Mwili wa marehemu Kalangula ulisafirishwa kwenda kwao Tukuyu mkoani Mbeya kwa mazishi yaliyofanyika Ijumaa liyopita. Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina.

Loading...

Toa comment