Deschamps Asema Pogba Hana Furaha Man United
KOCHA wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps, amesema kiungo wa Manchester United, Paul Pogba, hana furaha na nafasi anayochezeshwa kwenye timu hiyo na kumfanya ashindwe kuwika msimu huu.
Deschamps amemkingia kifua kiungo huyo, 27, kuwa alikuwa majeruhi kwa muda mrefu hivyo anahitaji muda wa kucheza ili kurejesha makali yake aliyokuwa nayo hapo awali. United inaonekana kukosa uwiano pindi wanapocheza na Bruno Fernandez, hivyo kumfanya Pogba kuanzia kwenye benchi.
Pogba yupo na timu ya taifa ya Ufaransa, kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Finland utakaochezwa leo usiku wakijandaa na mechi za Uefa Nations League dhidi ya Sweden na Portugal.