The House of Favourite Newspapers

Diamond Alamba Shavu Jingine WASAFI FESTIVAL – Video

MSANII  wa muziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul maarufu ‘Diamond Platnumz’, amesema haamini kuwa uhaba wa kondomu za kike ni chanzo cha maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi kwa kuwa si wote wawili wanaotakiwa kuvaa bali akivaa mmoja inatosha.

 

Ametoa kauli hiyo jana Jumatano Julai 10, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  baada ya kutangaza kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) katika kutoa elimu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi ambapo amesema wanaume ndiyo wanaowadanganya wanawake kuhusu matumizi ya kinga.

 

“Siamini kwamba kutopatikana kwa kondomu za kike kunachangia maambukizi kwa sababu si lazima wavae wote wawili, hivyo akivaa mmoja inatosha ni jambo la kueleweshana tu,” amesema.

 

“Sisi wanaume ndiyo tunaoongoza kulazimisha mtu asivae kinga, sasa dada zangu mjiulize ni kwa nini mtu afanye hivyo, maana yake hana nia nzuri na wewe itakuwa anataka upate ujauzito kwa lazima au nia nyingine mbaya na anakufanyia makusudi, ninaamini wanawake wakitusaidia kuweka misimamo kuwa haiwezekani basi haitawezekana,” amesema.

 

Kwa upande wake,  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa  Tacaids, Jumanne Issango, amesema kuna changamoto za upatikanaji wa kondomu za kike na kuwataka vijana kutotumia nafasi hiyo kama sababu ya kutoelewa na kutumia elimu zinazotolewa.

 

“Tunachokifanya ni kuwajengea uwezo wasichana kuweza kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao, wasichana wengi wasio na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wanawaachia mwanaume wamue iwapo watumie kinga au la, jambo ambalo tunapingana nalo sana hivyo tunawajengea uwezo wa kufanya maamuzi ya miili na afya zao kwa jumla,” amesema Issango.

 

“Maeneo kama Temeke, Kinondoni na mikoa mingine kuna makundi ya vijana ambao tunawajengea uwezo, tunaowaita wasichana balehe na wanawake vijana tunahakikisha wanapata elimu na kuwawezesha kiuchumi ili kuhakikisha wanapata elimu na kuwa na uwezo wa kujitegemea,” amesema Issango.

 

Tacaids wametangaza kushirikiana na kampuni ya Wasafi Ltd katika kupeleka ujumbe kwa jamii kuhusiana na suala la afya kupitia tamasha la Wasafi Festival ambapo wasanii watapata fursa ya kutoa elimu kwa vijana juu ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

TAZAMA VIDEO HAPA

Comments are closed.