The House of Favourite Newspapers

DIAMOND AMBADILI DINI KIM NANA

DAR ES SALAAM: Mzazi mwenzake mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Mondi’, Zarina Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ndio basi tena! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mwanamuziki huyo kudaiwa kumbadili dini mpenzi wake wa sasa, Video Queen, Lilian Kessy ‘Kim Nana’ ili afunge naye ndoa Amani lina Exclusive stori.  

Akizungumza na Amani, ndugu wa karibu na msanii huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina, alisema kuwa Diamond kwa sasa yupo na uhusiano ambao upo ‘siriasi’ kwani amefikia hatua ya kumbadili dini mpenzi wake huyo ili waingie naye kwenye ndoa.

MSIKIE NDUGU

“Nyie hamjui, wanaosema eti Kim Nana ametupiwa virago vyake nje huko Madale nyumbani kwa Diamond na mama yake, wamepitwa na habari, mwenzao Diamond kambadili dini anataka kumuoa kwani hata muda mwingi yupo na mama mkwe wake pale Madale.

“Hamjaona mara kwa mara anaonekana dukani kwa Esma, anachungwa utadhani ndio mwanamke wa kwanza kuwa na Mondi, yani Zari ndio basi tena,” alidai ndugu huyo wa karibu.

MONDI ANASEMAJE?

Gazeti hili la Amani, baada ya kupata ubuyu huo wa motomoto, lilianza kumtafuta Diamond ambapo simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa.

MAMA AMALIZA KILA KITU

Amani lilijiongeza na kumtafuta mama Diamond, Sanura

Kassim ‘Bi Sandra’ ambaye alianza kwa kufungukia skendo ya kumfukuza mwanadada huyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii hivi karibuni. Alisema ishu hiyo haina ukweli wowote kwani Kim Nana ndio ‘maza hausi’ kwa sasa na kudhihirisha hilo, yupo nyumbani hapo ambapo alimpa simu mwandishi azungumze naye kumhakikishia kuwa Kim yupo hapo.

AKIRI KUMBADILISHA DINI

Mama Mondi alieleza kuwa Kim yupo nyumbani kwake na sasa amebadilishwa dini na mwanaye ambapo anafundishwa kusoma Kuruani na mumewe Maisala Shamte ‘Anko’ na ndio maana wako karibu muda wote.

“Kwa taarifa yenu Kim nipo naye muda mwingi na sasa amebadili dini, anafundishwa Kuruani na mume wangu kwa hiyo watu watasubiri sana kama wanadhani ataachwa leo wala kesho, hilo halitatokea,” alisema mama Mondi. Baada ya mama Mondi kuongea hayo, mwandishi alimpasia simu Kim ambaye naye aliishia kucheka kwa furaha na akampa simu tena mama Mondi.

ANKO NAYE ATIA NENO

Baada ya simu kurejeshwa kwa mama Mondi, mwandishi wetu hakuishia hapo, alimuomba mwalimu wa Kurani, Anko Shamte ambaye naye alikiri kuwa karibu na Kim kwa ajili ya kumfundisha Kurani ikiwa ni pamoja na maadili na dini kwa ujumla. “Nipo naye karibu namfundisha maadili ya dini ya Kiislamu kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kusoma Kuruani kama alivyokwambia mama Diamond kwani kuna ubaya?” alihoji.

TUJIKUMBUSHE

Kim mara ya mwisho alikuwa akiishi Sinza, eneo la Mori ambapo alikuwa akiishi chumba kimoja, Gazeti dada na hili, Ijumaa lilimfungia kazi kuchunguza maisha yake ambapo liligundua kuwa anaishi kawaida kabla ya kuelezwa kuwa mrembo huyo amehamia Madale, nyumbani kwa Diamond.

WAPENZI ALIOTOKA NAO MONDI

Wanawake aliowahi kutoka nao Mondi ambao kila mmoja alijihakikishia kuolewa naye ni pamoja na Wema Sepetu, Penniel Mungilwa ‘Penny’, Zarinah Hassan ‘Zari’ na Hamisa Mobeto ambao wote kwa sasa hawana tena nafasi na kila mmoja ana maisha yake. Kati yao ni wawili tu waliofanikiwa kuzaa na Diamond ambapo Mobeto alimzalia mtoto mmoja huku Zari akimzalia watoto wawili.

Comments are closed.