The House of Favourite Newspapers

Diamond Atapiga ‘live’ Krismasi Dar Live

0

11899492_873726756045040_919698663_nMkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond.

Na Andrew Carlos
ISHU ni moja tu sasa, kwamba mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ atapiga show ‘live’ jukwaani kwa kutumia vyombo siku ya Krismasi kwenye Uwanja wa Taifa wa Burundani, Dar Live Mbagala, jijini Dar.

Diamond ambaye jana Ijumaa alitarajiwa kutambulisha ngoma yake mpya, atafanya show hiyo ukumbini hapo kuwashukuru mashabiki wake kwa mambo yote ya kumuunga mkono waliyomfanyia mwaka huu.

Licha ya kuonekana ni mateso kwa wasanii wengi hapa nchini, Diamond katika kinachoonekana kuwapa kitu halisia mashabiki wake, atapiga nyimbo zake kibao kwa kutumia vyombo kama vile vya bendi jukwaani.

Wakati akipiga show hiyo, Diamond anayetamba na nyimbo kibao ikiwemo ngoma ya Nana iliyotoka Mei mwaka huu, atakuwa bega kwa bega na wacheza show wake kuhakikisha anawapa kitu bora mashabiki wake.

Tuzo
Moja ya mafanikio aliyoyayapata Diamond mwaka huu kupitia Ngoma ya Nana ni kuibuka na tuzo kibao kama vile MTV Europe (EMA), African Music Magazine (Afrimma), Nollywood & African Films Critics (Nafca) na nyingine kibao ambazo baadhi yao zilikuwa katika kipengele cha Wimbo Bora wa Mwaka na Video Bora ya Mwaka.

Rekodi
Ngoma ya Nana imeweka rekodi katika mtandao wa Youtube kuwa miongoni mwa nyimbo za Diamond zilizotazamwa na mashabiki wake mara nyingi zaidi ikiwa ni mara 7,268,108.

Ngoma zake nyingine zilizotazamwa mara nyingi ni Mdogomdogo iliyotoka mwaka jana ambayo imetazamwa mara 5,086,813. Ntampata Wapi iliyotoka Desemba mwaka jana ambayo imetazamwa mara 6,597,653 pamoja na Nasema Nawe iliyotoka Aprili mwaka huu ambayo imetazamwa mara 5,531,289.

Ngoma mpya je?
Mashabiki wengi wa Diamond na muziki wa Bongo Fleva walitarajia kuisikia ngoma hiyo jana Ijumaa, ikiweka rekodi ya aina yake kwa kusikilizwa na kutazamwa mara nyingi zaidi ndani na nje ya nchi sambamba na kumletea mafanikio kama ilivyokuwa kwa Nana.

Akizungumzia ngoma mpya, Diamond alisema kuwa, kwanza itakuwa ni moja ya ngoma zake kali zote alizowahi kutoa.

“Kama ilivyo kawaida yangu sina maneno mengi, ngoma itajieleza yenyewe, na hii ni sapraiz kubwa kwa mashabiki wangu,” anasema Diamond.

Kuitambulisha Dar Live
Kwa mara ya kwanza baada ya kuachiwa ngoma hiyo mpya, Diamond ataizindua rasmi siku ya Krismasi yaani Desemba 25, mwaka huu ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.

Ikumbukwe kuwa mara ya mwisho kwa Diamond kufunika Dar Live ilikuwa Krismasi mwaka jana katika bonge moja la shoo lililokuwa likitambulika kama Usiku wa Wafalme akiwa na Mfalme Mzee Yusuf ambapo Diamond alikamua ngoma zake zote kali kama vile Ntampata Wapi, Mdogomdogo na nyingine kibao.

Msagasumu kama kawa
Katika kunogesha Sikukuu ya Krismasi Dar Live, mbali na Diamond kukamua na madensa wake, bingwa wa Muziki wa Singeli, Msagasumu naye atakuwepo jukwaani kukamua ngoma zake zote kali.

Mashabiki watarajie mperampera wa Msagasumu katika ngoma zake kali ambazo ni Inaniuma Sana aliyomshirikisha Juma Nature, Huyo Mtoto, Shemeji Unanitega, Naipenda Simba na nyingine kibao.

Wakali Dancers nao ndani
Mabingwa wa sarakasi, kucheza muziki wa kila aina, Wakali Dancers nao watakuwepo kukamilisha hamu ya mashabiki wa burudani ambapo watawaonesha mashabiki mbwembwe zote za mjini ikiwa ni pamoja na kujikunjakunja kwa staili kibao za sarakasi huku wakidansi ngoma za kisasa za ndani na nje ya Bongo.

Leave A Reply