The House of Favourite Newspapers

Diamond; kwa mafanikio gani hadi wakuonee wivu?

0

diamond (2)
N
ENO mafanikio lina maana pana sana na kwa mujibu wa wanasaikolojia, tafsiri sahihi ya neno hilo hubadilika kati ya mtu na mtu anayelihubiri au kuliishi.

Katika mfano mmoja wa kuchekesha sana, bosi wangu aliwahi kusema wapo baadhi ya watu, kuzungumza na mastaa wakubwa ni ndoto za maisha yao, kwa maana hiyo, hayo ndiyo mafanikio yao!

diamond (1)Maana nyepesi hapa ni kuwa mafanikio yako, siyo ya yule kwa sababu ndoto zinatofautiana. Unaweza kumuona mtu analala chini katika mabaraza ya majumba makubwa mtaa wa Samora, jijini Dar es Salaam ukawa unamhurumia, lakini kwake yeye, hayo ndiyo maisha bora kabisa ya ndoto zake, tofauti na kwao Mkumbi alikotoka!

Nimeanza hivi ili kujaribu kuzungumza na msanii mwenye jina kubwa kwa sasa hapa nchini, Diamond Plutnamz. Majuzi alirejea kutoka Marekani akiwa na tuzo tatu za Afrimma alizotwaa, akiwa mbele ya wenzake Vanessa Mdee na Ommy Dimpoz, waliopata tuzo moja moja.

Baada ya kupokewa na mamia ya mashabiki wake uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, msafara wao uliishia Escape One, ambako pamoja na kuzungumza nao, pia kulikuwa na burudani ya muziki. Ni katika mazungumzo yake, ndipo nilipopata wazo la kusema naye kwenye safu hii.

Diamond aliwaambia wanahabari kuwa wasanii wa Tanzania wanamuonea wivu kutokana na maendeleo yake kimuziki, ndiyo maana hakukuwa na yeyote aliyejitokeza kumuunga mkono siku hiyo, licha ya ukweli kuwa tuzo alizopata, sifa ni kwa Watanzania wote!

Kwanza nikiri kuwa mimi ni mmoja wa watu wanaofurahia jinsi Diamond anavyojitengenezea thamani katika muziki wake. Anajitahidi kufanya kila kitu kwa ubora, kuanzia uimbaji, madansa wake, video zake na mengineyo, kiasi cha kuwaaminisha wasanii wa nje kuwa yeye ndiye msanii bora kuliko wote Tanzania.

Hili ni jambo zuri, kwa sababu katika muziki wa biashara yenye ushindani kama wa sasa ulivyo, ubunifu ni kitu cha muhimu sana. Lakini hili la wivu kidogo linanitatiza.

Ninachojua mimi, Wabongo hatupendani, siyo kwa wasanii tu, bali hata wananchi wa kawaida mitaani. Na hali inakuwa mbaya zaidi unapoonesha dalili za kusogea kutoka hatua moja kwenda nyingine nzuri zaidi.

Lakini najiuliza, Diamond amefanikiwa kweli kwa kiasi gani hadi achukiwe na wenzake? Maana kuna tatizo pia, Mbongo mwenye mafanikio wenzake wakijitokeza kumuunga mkono, anabadilika na kujiona anapapatikiwa!

Ni kweli kwamba Diamond amekamata mpini miongoni mwa wasanii wa Bongo Fleva kwa umaarufu kwa sasa, lakini unadhani hakuna watu wanapiga hela kuliko yeye?

Kuna watu tunawajua wana miradi mingi iliyotokana na muziki, ambao huenda akaunti zao zinasoma kuliko tunavyofikiri, je, hawa nao wanamuonea wivu?

Dogo analo la kujifunza hasa kuhusu kauli anazozitoa mbele ya hadhara. Kama anadhani kuna siku wasanii wenzake watajikusanya na kumsifu kwamba yeye ndiye dira yao, naamini atasubiri sana kwa sababu siku hiyo haitatokea.

Anachopaswa kufanya ni kuendelea kupiga kazi na kuwaacha mashabiki waamue kuhusu nani ni nani.

Dawa ya Wabongo ni kuziba masikio na kufumba macho unapofanya mambo yako, ukitaka usikie wanachosema juu yako, au wanachokiona kwako, utaishia maumivu.

Maisha ya kusikilizia sifa yamepitwa na wakati, maana kama nilivyosema pale mwanzo, mastaa wa Kibongo kila mmoja anajiona yupo juu.

Leave A Reply