The House of Favourite Newspapers

Diamond, malizana na mshua bwana

diamond-platnumzNasibu Abdul ‘Diamond’.

KWAKO mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’. Bila shaka uko poa na unaendelea na shughuli zako kama kawaida. Natambua mchango katika kuhakikisha muziki wetu unasonga mbele, hongera kwa hilo.

Binafsi namshukuru Mungu amenijalia pumzi, maarifa. Nimeona si vibaya nikikukumbuka kwa barua maana kutokana na ubize wetu, ni nadra sana kuonana. Mara nyingi wewe unakuwa katika shoo zako za ndani na nje ya nchi, mimi kazi inanikaba koo kwelikweli.

BABADAbdul Juma ‘Baba Diamond’

Dhumuni la barua hii ni kutaka kukueleza kwamba, nimesikitishwa kuona tatizo lako na baba limechanua upya. Kwamba ‘mshua’ wako amefikia hatua ya kusema hata ikitokea Mungu amemchukua, usimzike maana haoni umuhimu wako.

Kwa waungwana, kauli hiyo si nzuri. Hata kama aliyeitamka ndiye chanzo cha tatizo lakini unapaswa kuitazama mara mbili. Najua kuna matatizo yaliyotokea nyuma ya sakata hilo lakini mwisho wa siku, mzazi ni mzazi tu.

Hata kama alikuudhi kiasi gani. Hata kama alikudharau kiasi gani, hata kama alikutelekeza, lakini unapopata mafanikio hauna budi kumsaidia. Kumbuka hata vitabu vya dini vinatukumbusha kuwa tusilipize baya kwa baya.

Hata kama mzee alikutendea ubaya, ili Mungu azidi kukubariki yakupasa umtendee wema. Mtendee mema kadiri ya uwezo wako. Si wakati wa malumbano kwani msaada anaoutaka yeye, haufanani hata kidogo na mafanikio yako.

Waswahili wanasema mzazi ni mzazi tu. Wazazi wengi waliwakosea watoto wao, ama kwa makusudi na kutojali, au kwa kutojua. Ruhusu moyo wako uwe mweupe na yeye afurahi. Akifurahi yeye kwa kile kidogo utakachomsaidia, Mungu atakuzidishia zaidi.

Tunayo mifano mingi ya mastaa ambao walitofautiana na wazazi wao na kujikuta wakiangukia kwenye balaa. Sikuombei hivyo, lakini pia yakupasa ujifunze kwamba mzazi ni mzazi tu hata iweje. Kwani atakupunguzia nini ukimpa hata laki mbili tu kwa mwezi?

Unaingiza shilingi ngapi wewe? Fedha kiasi gani unazipoteza katika kufanya maisha ya kawaida kama vile bethidei na mambo mengine yanayofanana na hayo? Mbona ulimnunulia hata gari la kutembelea mdogo wako Queen Darleen, utashindwa kiasi hicho kidogo cha fedha?

Mjengo unaoishi wewe na mama yako haufanani hata kidogo. Wako ni wa kitajiri, wa mzee ni wa kawaida. Kwa nini usifanye kitu hapo? Yote kwa yote, busara na hekima zako ndizo zitakusaidia katika hili, hivyo mimi nakusihi malizana na baba’ko.

Najua suala la kumsaidia mzazi huyo kwako ni dogo sana, fanya hivyo basi na mzee aache kulalamika katika vyombo vya habari, kitu ambacho kinaweza kukuharibia wewe na mashabiki wanaofuatilia muziki wako mzuri.

Ni matumaini yangu kwamba utalitilia maanani jambo hili na Mungu akutangulie katika utekelezaji wake, ishallah lipite salama.
Ni mimi mtu wako wa nguvu,

Comments are closed.