DIARY ya Shigongo – 42: Umejiandaaje na Baada ya Kustaafu na Kuzeeka?

NI Jumamosi tulivu ninapoandika makala haya, nipo ofisini kwangu nikiendelea na majukumu yangu ya kila siku.

 

Ijumaa iliyopita, nilipata bahati ya kipekee ya kuzungumza na ndugu zangu, wanaushirika wa Chama cha Kuweka na Kukopa cha Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA -SACCOS). Walinialika ofisini kwao, Mawasiliano Tower jijini Dar es Salaam.

 

Tulizungumza nao mambo mengi, lakini kubwa likiwa ni jinsi ya kujiandaa unapoelekea katika umri wa kustaafu na kuzeeka. Kutokana na umuhimu wa kile tulichozungumza na ndugu zangu hawa, leo napenda kuzungumza nawe msomaji wangu kupitia ukurasa huu.

 

Hebu nikuulize msomaji wangu, kama wewe ni mwajiriwa iwe ni serikalini, kwenye mashirika au kampuni binafsi, unajua kwamba kuna siku utastaafu na hutakuwa tena na uwezo wa kufanya kazi?

Hata kama hujaajiriwa, pengine umejiajiri mwenyewe kwenye shughuli zako, unatambua kwamba itafika siku hutaweza tena kufanya shughuli zako kama kawaida kutokana na kuzeeka na kuishiwa nguvu?

Ni kawaida kwa binadamu kuzaliwa, kukua, kuzeeka kisha kufa, lakini ni wangapi huwa wanakumbuka kufanya jambo leo wangali na nguvu, kwa ajili ya kesho watakapokuwa wamezeeka?

Ukishajua kwamba itafika siku utastaafu, hutakuwa tena na uwezo wa kufanya mambo ambayo unaweza kuyafanya kwa sasa, ndipo utakapojua kwamba kuna umuhimu wa kuanza kujiandaa leo ili kesho yako iwe nyepesi.

 

Upo ushahidi wa watu ambao kwa miaka mingi walilitumikia taifa hili kwenye nyanja mbalimbali, lakini siku walipostaafu tu, maisha yao yote yakaharibika kabisa. Umezoea kupokea mshahara kwa kuwa unafanya kazi, kesho hutakuwa na kazi tena kwa sababu umestaafu, utawezaje kuendesha maisha yako?

 

Tunayo mifano ya wastaafu wetu wengi ambao hawakufanya maandalizi mapema, walipostaafu wakapokea pesa zao za kiinua mgongo na wakashindwa wafanye biashara ipi. Wengine hukurupuka kufanya biashara ambazo hawazijui vizuri na mwisho wa siku wanaishia kufilisika, kupata presha na kufa mapema.

Umezoea kujiingizia kipato kwenye shughuli unazozifanya, iwe ni biashara, kilimo au shughuli yoyote, kesho umezeeka, huna tena nguvu za kuweza kukimbizana mitaani kutafuta riziki, familia yako itaishije?

Jambo la msingi unapaswa kuanza kufanya maandalizi leo na usisubiri mpaka utakapostaafu au kuzeeka ndipo uanze kujiandaa, wakati ni sasa.

Pengine unaweza kuwa unajiuliza, natakiwa kufanya nini ili maisha yangu ya uzeeni baada ya kustaafu kama Mungu akinipa umri mrefu yawe mepesi?

 

Jambo la kwanza na la muhimu, ni kuanzisha vyanzo vingi vya mapato badala ya kutegemea mshahara peke yake. Jiulize hapo ulipo leo, itakuwaje siku ukiamka huwezi tena kufanya kazi kama unavyofanya sasa hivi, maisha yako yatakuwa yaleyale? Utaendesha gari lilelile? Watoto wako utawapeleka shule ileile? Ili tufanikiwe, tusiamini katika chanzo kimoja cha mapato.

Unaweza kuwa ni mwajiriwa, lakini ukaanzisha biashara yako nyingine ndogo huko mtaani, ukaweka mtu makini na ukaingiza fedha. Biashara hiyo ikisimama vizuri unaanzisha nyingine. Lazima baada ya miaka minne hadi kumi upate mafanikio.

 

Hata ikija kutokea umestaafu, kwa kuwa tayari ulishaanza kujenga misingi ya biashara tangu mwanzo, fedha utakazozipata unaweza kuzitumia kupanua biashara ambazo tayari una uzoefu nazo na unaelewa jinsi mzunguko wake wa fedha ulivyo.

 

Siyo lazima ufanye kila kitu wewe mwenyewe, tafuta watu waaminifu na anza kufanya nao kazi leo ukiendelea kuwapima uaminifu wao, hao ndiyo watakaokusaidia hata pale utakapokuwa huna nguvu tena kwa sababu ya uzee.

Jambo lingine muhimu, ni kuwekeza katika afya yako kwa kula vizuri lishe bora, kufanya mazoezi na kufanya vipimo na uchunguzi wa afya ili kuhakikisha upo imara.

Lazima afya yako uijali, hiyo ndiyo inayokupa nguvu za kufanya kazi. Uzeeni kuna magonjwa mengi, kisukari, tezi dume, shinikizo la damu na magonjwa mengine, lazima uwe na utamaduni wa kuwekeza katika afya ili uendelee kuwa na nguvu ya mwili na akili wakati ukitekeleza majukumu yako.

 

Pia unapaswa kuwekeza kwa watoto wako kwa kuwapa elimu iliyo bora kwani utakapozeeka, watoto wao ndiyo watakuwa na jukumu la kukulea, hivyo ukiwaandalia maisha mazuri leo, utalelewa kwa furaha katika uzee wako kwani watoto tayari watakuwa na maisha yao mazuri.

 

Mpe elimu bora mwanao, wakati mwingine mpitishe katika shida ili ajifunze kuishi na watu, ajifunze changamoto na jinsi ya kuzitatua. Ukiwa na maisha mazuri halafu mwanao ukamwacha akavuta unga tambua kwamba unaandaa ‘time bomb’, unaandaa bomu litakalokuja kukulipukia mwenyewe.

Watengeneze wanao waje kuwa raia wema watakaoitetea nchi yao na kupigania mafanikio yao na ya taifa.

Jambo lingine muhimu ambalo wengi huwa wanalisahau, ni kuwekeza katika watu. Wainue vijana wadogo kwenye idara yako au mtaani mwako, waweze kufikia malengo yao. Wala usibague, wasaidie hata wale ambao siyo ndugu zako kwa sababu siku ukichoka hawa ndiyo watakaokusaidia.

 

Pia jifunze kuanzisha biashara zisizo na purukushani. Kwa mfano, unaweza kununua kiwanja eneo la karibu na barabara au sehemu iliyochangamka, jenga ‘fremu’ za maduka na uzipangishe, utakuwa unaingiza fedha kwa miaka mingi ijayo hata ukiwa umelala.

 

Chagua biashara chache unazoweza kuzifanya kwa ukamilifu. Watu wengi huwa wanakwama kwenye biashara kwa sababu unakuta mtu anataka afanye kila biashara. Huwezi kufanikiwa katika hilo. Chagua maeneo machache unayoyamudu vizuri, chagua kitu ambacho kinatatua kero za watu halafu wekeza nguvu zako hapo, hakika utafanikiwa.

Ukishajiimarisha katika biashara anza kutumia mabenki na taasisi za fedha kukopa na kuendeleza biashara zako, hakuna tajiri hata mmoja asiyekopa. Watu wengi ambao huingia kichwakichwa kwenye mikopo ya mabenki, ndiyo wale ambao miaka michache baadaye utasikia nyumba yake inapigwa mnada kwa sababu ameshindwa kulipa.

 

Usikope kwa ajili ya kwenda kuanzisha biashara mpya! Kopa ili kuendelea biashara ambayo tayari ulishaianzisha na unaelewa vizuri jinsi mzunguko wake wa fedha unavyokuwa. Usikope ili kwenda kujenga heshima baa au ili kwenda kuongeza wake wawili au watatu! Matokeo yake hayatakuwa mazuri.

Usisahau kumtanguliza Mungu kwa kila unachokifanya. Muombe Mungu kila siku akupe maisha marefu na afya njema, iombee familia yako na pia toa kile Mungu alichokujaalia kwa ajili ya kuwasaidia wenye uhitaji.

Jenga utaratibu wa kwenda kutoa misaada kwa watoto yatima, wajane au watu wanaoishi kwenye mazingira magumu na hakika Mungu atakubariki.

Ukiyazingatia yote hayo, hakika hutaogopa kustaafu wala hutaogopa kuzeeka! Nakusisitiza kwamba anza leo kabla hujachelewa na Mungu akubariki sana.

Ahsanteni kwa kunisoma. Tukutane wiki ijayo.


Loading...

Toa comment