The House of Favourite Newspapers

Dilunga: Sasa Gari Ndo Limewaka

0

HASSAN Dilunga, yule fundi wa Simba anayevaa jezi namba 24, ametamka kwamba yale mawili aliyotupia hajabahatisha, sasa gari ndio limewaka.

 

Katika mechi mbili mfululizo dhidi ya Mbao na Alliance, Dilunga alitupia na amesisitiza kwamba mfumo wa Mbelgiji, Sven Vanderbroeck umemnogea.

 

Dilunga ambaye amewahi kuzichezea Yanga na Mtibwa, chini ya kocha huyo mpya wa Simba, aliyejiunga mwishoni mwa mwaka jana amefunga mabao manne na kutoa pasi moja ya bao jambo linalomfanya kuwa na kiwango kizuri zaidi kwa sasa.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Dilunga alisema kuwa ana furaha kupangwa katika nafasi ya kiungo wa pembeni na kocha wake kwani nafasi hiyo inampa fursa ya kufunga zaidi mabao na kama akiendelea kupangwa basi atazidi kufunga kadiri atakavyopata nafasi.

 

“Ninafurahia hii nafasi ambayo kocha ananipanga, inanipa fursa ya kufunga mabao na unaona jinsi gani kila nikipata nafasi najitahidi niweze kufunga, kikubwa ni kupata nafasi ya kucheza zaidi na ikitokea napata nafasi ya kucheza basi natakiwa nijitahidi kufunga.

 

“Hapa kuna wachezaji wengi zaidi na walio bora katika kila nafasi, hii inanifanya nigundue kuwa ili upate nafasi basi inakubidi upambane haswa, sichukii kuzungukwa na wachezaji bora bali nachukulia kama changamoto kwangu ili nizidi kuwa imara,” alisema Dilunga ambaye alivunja mkataba na Yanga mwaka 2015.

Leave A Reply