The House of Favourite Newspapers

VIDEO: DINI YA AJABU YAIBUKA DAR, WAUMUNI WAKE HAWAAMINI KIFO!

DUNIA ina mambo! Ukiambiwa kuna imani ya dini inayofundisha waumini wake kwa kutumia vitabu viwili vitakatifu vya Biblia na Quran kwa wakati mmoja, utashangaa. Hiyo ndiyo dini ya ajabu iliyoibuka Bongo, ambapo kiongozi wake, aliyejitambulisha kwa majina mawili – Nabii Eliya au Nabii Ilyaas anatoa huduma hiyo maeneo ya Misugusugu, wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani.

 

Gazeti hili linamuibua nabii huyo, ikiwa ni siku chache tangu mtu mmoja, aitwaye Michael Job ambaye hujiita Yesu, alipokamatwa nchini Kenya na kurudishwa kwao Marekani.

 

Ilielezwa kuwa, jamaa huyo alialikwa nchini Kenya na mchungaji mmoja ambaye hakutajwa jina wala kanisa lake, ambapo alikuwa akipita mitaani na kuwaaminisha watu kuwa yeye ni Yesu Kristo na angewapeleka mbinguni. Job ambaye ni mwigizaji wa Hollywood, nchini Marekani alikuwa akipita mitaani huko Kenya na kukusanya fedha kama sadaka kabla ya kudakwa na kurudishwa kwao hivi karibuni, lakini mchungaji aliyemwalika akatiwa nguvuni.

 

DINI YA AJABU BONGO Risasi Jumamosi lilipokea malalamiko kutoka kwa chanzo chetu, ambacho kilipiga simu katika chumba cha habari cha gazeti hili, kikieleza kuwepo kwa dini hiyo, maeneo ya Misugusugu Karabaka na kuwapa usumbufu mkubwa raia. “Jamani huku Misugusugu sisi wananchi wa hapa Misugusugu Karabaka, kuna nabii ambaye hatumuelewi.

 

Amefungua sijui ni msikiti, sijui ni kanisa na anafundisha watu kwa kutumia Biblia na Quran kwa wakati mmoja. “Waumini wake wanavaa kanzu kama Waislam, lakini mambo yao ndiyo yanayotukera. Maombi wanayofanya hatujui ni ya aina gani, maana wanaimba usiku kucha.

 

“Kuna wakati utawasikia wanaimba kama Waislam, wakati mwingine kama Wakristo kwa kiswahili cha kawaida. “Kuna wakati usiku huwa wanakimbiakimbia kama wanafanya mazoezi. Sisi majirani hatuwaelewi wako upande gani na wala hatujui huwa wanakula muda gani maana wapo bize muda wote,” kilieza chanzo hicho.

 

MGONJWA AFARIKI WAKIMUOMBEA

Kikiendelea kutiririka chanzo hicho kinasema kuwa, kuna wakati mgonjwa alipelekwa kwa Nabii Eliya kuombewa, akafariki dunia kisha wakaanza kumuombea afufuke bila mafanikio. “Huyo mgonjwa alikuwa mwanamke, anaitwa mama Halima. Alipelekwa na mume wake. Wote ni waumini wake,
lakini katikati ya maombi, huyo mama akafariki dunia.

Nasikia wanadai hawaamini kifo, kwa hiyo wakaanza kumuombea wakiwa wameifungia maiti ndani.

“Ilibidi majirani tushirikiane, tumuite mwenyekiti wa serikali ya mtaa, naye akaita polisi ndipo maiti ikatolewa kwenda kuzikwa huku ikiwa imeanza kuharibikia. Kwa kweli ni dini ya ajabu sana. Njoeni wenyewe mjionee,” kilisema chanzo hicho.

 

RISASI ENEO LA TUKIO

Timu ya waandishi wa Risasi Jumamosi ilifunga safari hadi Misugusugu na kufika hadi eneo iliyopo nyumba ya kuabudia na kufanikiwa kukutana na Nabii Eliya na waumini wake. Akizungumza kwa kujiamini, ‘Nabii’ Eliya alisema ni kweli anatoa huduma ya imani hiyo kwa watu wa dini zote mbili – Wakristo na Waislam, pia wasiokuwa na dini.

 

“Nimeanza kutoa huduma hii miaka mitano iliyopita, siyo kanisa kama wanavyodai hao wananchi. Mimi natoa huduma ya maombi, bado sijafungua kanisa ila nina wanafunzi ambao nawafundisha namna ya kumjua Mungu na kuwa na imani thabiti juu ya Mungu.

 

“Nawafundishia nyumbani kwangu, kwa kuwa jumba la kifalme bado sijakabidhiwa. Nasubiri Mungu anipe kibali, Rais Dk. John Pombe Magufuli ahame Dar na kwenda Makao Makuu Dodoma, ndipo watu wa Mungu watahamia pale (Ikulu ya Magogoni) wakimngojea Yesu Kristo.

 

Hapo namaanisha kuwa Ikulu itakuwa ni Jumba la Kifalme,” alisema Nabii Eliya. Risasi Jumamosi: Kwa nini umejitambulisha kwa majina mawili ya Nabii Eliya na Nabii Ilyaas kwa wakati mmoja? Nabii Eliya: Ni kwa sababu nahubiri dini zote mbili kwa wakati mmoja. Jina moja la Kiislam, jingine la Kikristo.

 

Natumia Biblia na Quran kufundishia. Unajua mwanzo mimi nilikuwa Muislam, lakini niliitwa na Yesu Kristo kwa ajili ya kuja kutoa huduma hii. Risasi Jumamosi: Inasemekana imani ya dini unayoihubiri haiamini kifo ni kweli? Nabii Eliya: Kweli kabisa, siamini katika kifo, namaanisha hakuna kifo.

 

Kama umemkiri Yesu kuwa Bwana na Mwokozi huwezi kufa, kwa hiyo nimekuja kufunga kifo kwa kila mwanadamu ambaye atakubali mafundisho yangu hawezi kufa.

 

“Mimi na wanafunzi wangu hatuwezi kufa, tutaishi milele mpaka Yesu atakaporudi. Nina wanafunzi kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni, ikiwemo Dubai, Ujerumani, India, Marekani na kwingineko, hivyo nawakaribisha wote wajiunge nasi hawatakufa.

“Mimi baba yangu mzazi amefariki dunia siku si nyingi, lakini sikwenda kwenye msiba kwa kuwa siamini kifo.

 

Risasi Jumamosi: Tumesikia habari ya kumuombea mama mmoja aitwaye mama Halima na akafariki dunia ni kweli? Nabii Eliya: Kweli kabisa.

 

Risasi Jumamosi: Kama unafundisha imani ya kutoamini kifo na umesema wewe na waumini wako hamtakufa, imekuwaje mama Halima akafariki dunia?

 

Nabii Eliya: Kwanza huyo mama Halima hakuwa muumini wangu, mumewe ndiye tunaabudu naye hapa. Huyo marehemu alikuwa na ugonjwa wa kifafa, mume wake alimleta ili tumfanyie maombi, kwa kuwa hakuwa amemkiri Yesu Kristo, umauti ukampata. Mambo mengine aulizwe mumewe huyo marehemu, mimi siwezi kujua.

 

Risasi Jumamosi: Mbona mnavaa kanzu kama Waislam? Nabii Eliya: Sisi tunavaa mavazi ambayo Yesu Kristo alikuwa akivaa, hatukatazi kuvaa suti lakini Yesu hakuvaa suti.

 

MJUMBE AFUNGUKA Baada ya kumaliza mahojiano na Nabii Eliya ambaye imani yake inaonekana kuwashangaza wengi, waandishi wetu walimhoji Mjumbe wa Shina namba 2 wa Mtaa wa Karabaka, Mohamedi Mbena na kumwuliza kuhusiana na malalamiko ya wananchi wake juu ya huduma inayotolewa na nabii huyo.

 

 

“Napata malalamilo kuhusu huyo Nabii Eliya, wananchi wanalalamika kupigiwa kelele usiku, lakini pia wazazi wanadai watoto wao huchelewa kurudi majumbani wakitoka shule, maana hupitia pale kwake na kuwashangaa kwa sababu wanafanya shughuli zao nje wakati mwingine,” alisema Mbena. Mjumbe huyo amesema kuna wakati wananchi waliandamana wakimpinga, hali iliyomlazimu kuita polisi kutuliza ghasia.

Comments are closed.