The House of Favourite Newspapers

Djuma Avunja Rekodi ya Usajili Bongo

0

 

DEAL DONE! Ndivyo utakavyoweza kusema hivi sasa ni baada ya mabosi wa Yanga kufanikisha usajili wa beki wa kulia wa AS Vita, Shaban Djuma, kwa dau linalokadiliwa kufikia Sh milioni 500.

 

Yanga imefanikisha usajili huo juzi Jumatano baada ya Makamu wa Kamati ya Mashindano na Usajili wa Yanga, Injinia Hersi Said kusafiri kwenda nchini DR Congo kufanikisha usajili wa nyota huyo.

 

Timu hiyo ilikuwepo kwenye mipango ya muda mrefu ya kufanikisha usajili wa beki huyo ambaye inaelezwa klabu kubwa za TP Mazembe, Al Ahly na Mamelodi Sundowns zilikuwa zikiwania saini za nyota huyo.

 

Kabla ya Djuma wachezaji wengine waliokuwa wanaongoza katika usajili ghali ni Wakongomani Tuisila Kisila, Mukoko Tonombe ambao dau lao lilifikia Sh 250Mil wakitokea AS Vita, Mrundi Said Ntibazonkiza ‘Saido’ Sh 150Mil kwa upande wa Simba wapo Mzambia Clatous Chama Sh 300Mil na Luis Miquissone Sh 173.4Mil.

 

 

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka kwa mmoja wa mabosi wakubwa wenye ushawishi wa timu hiyo, Yanga imefanikisha usajili huo kwa asilimia mia moja baada ya kufikia makubaliano mazuri na meneja wa Djuma.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Djuma amesaini mkataba wa miaka miwili huku dau lake likitajwa kuwa si chini ya Sh 500Mil. Ni rekodi kubwa ya usajili ambayo haijawahi kutokea kwa mchezaji kuwahi kusajiliwa katika Ligi Kuu Bara.

 

Aliongeza kuwa, Injinia pia alikuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa FC Lupopo, Ciel Ebengo Ikoko.

 

“Yanga tumepania hivi sasa katika usajili wetu na hiyo ni katika kutengeneza kikosi imara kitakachofanya vema katika michuano ya kimataifa ambayo mwakani tutashiriki,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Hersi akiwa Congo jana saa mbili asubuhi, alitupia picha akiwa na Waziri wa Michezo wa nchi hiyo, Serge Konde na kuandika ujumbe uliosomeka hivi: “Nikiripoti kutoka hapa KINSHASA ni mimi Eng. DJUMA HERSI SHABANI wa @yangasc.”

STORI: WILBERT MOLANDI,Dar es Salaam

Leave A Reply