The House of Favourite Newspapers

Dk Magufuli: Ajenda ni maendeleo, si kushabikia vyama

0

Magufulii

Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli.

Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amewataka Watanzania kuweka vyama vyao pembeni, badala yake kuweka mbele ajenda ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika jimbo la Buyungu, wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma, Dk Magufuli alisema vyama vya siasa siyo maendeleo ya wananchi, bali wananchi wanahitaji maendeleo zaidi ya vyama vyao.

Alisema Serikali yake itasimamia zaidi shughuli za maendeleo ili Watanzania waone shughuli zinazofanywa na Serikali yao. Alisema anakusudia kujenga Tanzania mpya yenye watu wanaofanya kazi kwa bidii.

“Ninataka tuweke vyama vyetu pembeni, maendeleo mbele; makabila yetu pembeni, maendeleo mbele; dini zetu pembeni, maendeleo mbele,” alisisitiza mgombea huyo huku akiitikiwa na wananchi waliokuwa wakimsikiliza.

Mgombea huyo aliahidi kuubadilisha mji wa Kakonko kupitia miradi mbalimbali ya umeme na barabara itakayoanza kutekelezwa mwakani.

Aliahidi kilomita tatu nyingine za barabara ya lami kwa halmashauri ya Kakonko.

“Ninatambua tatizo la soko la tumbaku na mazao ya ngozi kwa wananchi, jambo linalowafanya washindwe kunufaika na mazao yao. ninaahidi kuwa Serikali yangu itaanzisha viwanda vya sigara, nyama na viatu.

“Watu wa Kakonko mna bahati kubwa, mmepewa wilaya wakati mna watu karibu 160,000. Naomba mumchague tena mbunge wenu, Christopher Chiza ili nishirikiane naye kuwaletea maendeleo,” alisema Dk Magufuli wakati akimwombea kura aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma, Dk Amani Kabourou alisema kwa muda mrefu mkoa huo umekuwa kichwa cha mwendawazimu kwa sababu majimbo matano yalishikiliwa na vyama vya upinzani.

Aliwataka wananchi hao kutorudia makosa kwa kuchagua upinzani, badala yake wachague wagombea wa CCM ili washirikiane na Dk Magufuli endapo naye atachaguliwa kuwa Rais wa nchi hii.

Awali Dk Magufuli alikwenda kuhani msiba wa mwalimu wake, Cornel Pastory aliyefariki dunia Agosti 7, mwaka huu, Biharamulo, mkoani Kagera.

Mwalimu Pastory ndiye aliyempokea Dk Magufuli alipokwenda kuandikishwa darasa la kwanza katika shule ya msingi Chato, mwaka 1966.

Dk Magufuli alifika nyumbani kwa mwalimu huyo katika kitongoji cha Kanywamaizi saa 7.45 mchana na kushiriki ibada fupi ya kumwombea mwalimu huyo.

Baada ya ibada hiyo, Dk Magufuli alikwenda kuweka shada la maua kwenye kaburi la mwalimu huyo aliyezikwa katika uwanja wa nyumbani kwake.

Baada ya kuweka maua na kufanya sala fupi kwa marehemu, mgombea huyo aliendelea na ziara yake ya kampeni katika uwanja wa Biharamulo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Dk Magufuli alionyesha kusikitishwa na kifo cha mwalimu wake kiasi cha kushindwa kuendelea kumzungumzia.

“Historia ya maisha yangu imetokana na Biharamulo, leo nimefika nyumbani kwa mwalimu wangu aliyenipokea darasa la kwanza, kwa kweli…” alisema Dk Magufuli na kutulia kwa sekunde kadhaa kabla ya kuendelea kuzungunzia mambo mengine.

Mgombea huyo aliwaambia wananchi wa Biharamulo kwamba anakusudia kuinua maisha ya wananchi kwa kuanzisha viwanda vya nyama na viatu, ili waweze kuuza mifugo yao na ngozi kwenye viwanda hivyo.

(CHANZO: MWANANCHI)

Leave A Reply