NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson Mwansasu, amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli (JPM), inalenga zaidi kwenye matokeo ya utekelezaji wa miradi mikubwa, ikiwemo ununuzi wa ndege.
Dk Tulia amesema Rais Magufuli ni mtu anayependa kuona mambo mliyokubaliana yakitendeka badala ya maneno tupu na ndiyo maana katika utawala wake, mambo makubwa ambayo awali yalikuwa hayawezekani, sasa yanatekelezwa na Serikali yake.
Dk Tulia ameyasema hayo mapema leo asubuhi alipotembelea ofisi za Global Group zilizopo Sinza-Mori jijini Dar, kampuni inayohusika na uendeshaji wa mtandao huu, Chaneli ya Global TV Online na wachapishaji wa Magazeti ya Championi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Amani, Risasi, Uwazi, Spoti Xtra na Betika na kuongeza kwamba watu wanaopinga hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli, wanatakiwa kuelimishwa.
“Tukizungumzia ununuzi wa ndege kwa mfano, baadhi ya watu wanaweza kuhoji kwamba tutanufaika nini na ndege bila kujua kwamba zitatumika kuwaleta watalii ambao wataleta fedha nchini kwetu ambazo zitasambaa kwenye mzunguko na kumfikia kila mmoja.
“Mfanyabiashara anataka wateja, wafanyakazi wanataka mishahara, hizo fedha zote lazima ziwepo kwenye mzunguko na watalii watakaoletwa na ndege zetu ndiyo watakaoingiza fedha hizo, kwa hiyo ni suala la kuelimishana tu, lakini ninampongeza sana mheshimiwa Rais kwa hatua anazozichukua.
“Mtu mwingine anaweza asione umuhimu wa ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge wakati anatumia umeme, hata yule ambaye anatumia mafuta ya taa ili apate mafuta ni lazima yasafirishwe, lazima yapite kwenye barabara, kwa hiyo utagundua kwamba juhudi za mheshimiwa Rais zinagusa maisha ya watu wengi zaidi,” alisema Dk Tulia.
PICHA: MUSA MATEJA na SWEETBERT LUKONGE | GLOBAL PUBLISHERS
Comments are closed.