Dkt. Abbasi Akutana na Rais Tuzo za Utalii za Dunia, Tanzania Kuandaa za Afrika 2025
Siku moja baada ya Tanzania kutwaa Tuzo ya Dunia ya Sehemu Maridhawa Zaidi kwa Utalii wa Safari 2024 (World’s Leading Safari Destination), mikakati imeanza ili Tanzania kuandaa Tuzo hizo ngazi ya Bara la Afrika mwakani.
Hayo yamejadiliwa wakati wa kikao kati ya Rais wa Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards, WTA), Bw. Graham Cooke kutoka nchini Uingereza, alipokutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutoka Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi mjini hapa leo.
Itakumbukwa usiku wa kuamkia leo pamoja na kuwa nchi pekee kutoka Bara la Afrika kushinda tuzo katika tukio la mwaka huu lililohudhuriwa na wadau wa utalii na biashara takribani 500 duniani, Tanzania pia ilitangazwa kuwa mwenyeji wa Tuzo hizo kwa ngazi ya Bara la Afrika na Ukanda wa Nchi za Bahari ya Hindi (World Travel Awards Africa & Oceanic Gala 2025).
“Fursa hii ya kuwa mwenyeji itaisaidia Tanzania kujitangaza zaidi duniani kwani itatajwa sana katika majarida na mitandao mikubwa ya utalii duniani na katika kila tukio la WTA katika mabara mengine Tanzania itaonekana,” alisema Bw. Cooke mwanzilishi wa Tuzo hizo.
Mbali ya WTA, Bw. Cooke ni mwanzilishi na Rais wa Kampuni ya Virtual World Internet inayosifika katika kutumia mtandao kutangaza utalii (internet virtual images) na pia mmiliki wa moja ya taasisi kubwa za habari za utalii ya ‘Breaking Travel News’ zote zikiwa na makao makuu yake nchini Uingereza.
“Katika mazungumzo yetu kwanza ameisifu Tanzania kuwa nchi yenye vivutio vya kipekee lakini akasema juhudi za sasa za kujitangaza zaidi zinapaswa kuendelezwa hasa kutumia njia za kisasa za kidijiti ikiwemo matumizi ya akili bandia moja ya eneo ambalo kampuni zake zimebobea katika utafiti na maendeleo.
“Aidha, ameahidi kutusaidia kujitangaza kupitia kampeni aliyoibuni iitwayo ‘Seven Wonders’ inayokwenda zaidi ya kutangaza ‘top five’ ya wanyama tulionao,” ameeleza Dkt. Abbasi baada ya kikao hicho.