The House of Favourite Newspapers

Dkt. Abbasi: Serikali Inakuja na Tamasha, Tuzo Kubwa za Sanaa

0

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbas, jana Desemba 2, 2020,  ametangaza kuwa serikali ikishirikiana na wadau itaratibu tamasha kubwa la aina yake la muziki na sanaa litakalotumia jina la moja ya vivutio vikubwa vya utalii hapa nchini.

 

Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika siku ya tatu ya ziara yake ya kukutana na wadau wa sanaa  katika kuhimiza  urithi mkubwa wa sanaa  nchini ukiwemo muziki, filamu, ngoma  na nyinginezo, ambapo alisema sekta hiyo inapaswa kuhakikisha inaiburudisha jamii yetu ya wachapakazi ipasavyo.

 

Aidha, amesema kuanzia mwakani serikali pia itashirikiana na wadau kurejesha tuzo za muziki na sekta nyingine za wizara hiyo.

 

“Moja ya kazi kubwa za sekta ya sanaa nchini ni kuhakikisha jamii yetu inayochapa kazi sana kwa sasa inaburudika ipasavyo.  Sasa naona sanaa inakuja tu pale panapokuwepo mdhamini au mwandaaji fulani,  asipokuwepo hakuna matukio na nchi iko kimya,” alisema.

 

Serikali sasa inakwenda kuchangamsha  sekta hii kwa kuratibu tamasha kubwa sana litakaloanzia Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam na kuendelea kuungana na Tamasha la Kimataifa la Sanaa Bagamoyo.

 

“Wasanii wakiungana watajaza uwanja,  tutateremsha wasanii wetu wote ambao ni urithi wa sasa na baadaye wa nchi hii halafu tuone kama watu hawatakuja,” alisema.

 

Leave A Reply