The House of Favourite Newspapers

Dkt. Biteko Afungua Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Africa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akifungua Mkutano wa Nishati Barani Afrika (Africa Energy Summit, 2025) leo Januari 27, 2025 unaoendelea katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Kama ilivyobainishwa katika Ajenda ya Afrika 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), leo Dar es Salaam inayo heshima ya kuwa mwenyeji wa wajumbe kutoka Afrika na kwingineko, wakihudhuria Mkutano huu muhimu unaolenga kuimarisha azma ya Afrika ya kuipatia bara hili nishati.

Baada ya kupata Uhuru mwaka 1960, nchi za Afrika zimepiga hatua kubwa katika kuzalisha na kusambaza umeme kwa wananchi wao. Tanzania ilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 21 pekee wakati wa Uhuru, kwa sasa nchi ina uwezo wa kuzalisha megawati 3,160.

Pamoja na mafanikio makubwa ya kuzalisha umeme barani Afrika, takriban Waafrika milioni 571 bado hawana huduma ya umeme. Mkutano huu umeitishwa rasmi kwa lengo la kujadili namna ya kuongeza upatikanaji wa umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Natoa shukrani za dhati kwa waandaaji wenza wa Mkutano huu ikiwemo: Benki ya Dunia; Benki ya Maendeleo ya Afrika; Rockefeller Foundation; Sustainable Energy for All (SEforALL), na The Global Energy Alliance for People and Planet (GEAPP) kwa ushirikiano uliowezesha kufanyika kwa Mkutano huu.

Uwepo wenu, mawazo na utaalamu wenu ndiyo vitakavyofanikisha Mkutano huu. Natarajia majadiliano yenye tija na tushirikiane katika kuunda mustakabali wa nishati barani Afrika.

Natarajia mkutano huu utakuwa ni hatua muhimu katika kufanikisha lengo letu la upatikanaji wa umeme kwa wote.

Katika mkutano huu, Mawaziri wa Nishati, Viongozi wa Taasisi za Kimataifa za Kifedha, Wataalam na Wadau wa Mashirika ya Kiraia, watapata fursa ya kujadili na kukubaliana malengo, vipaumbele vya sera, suluhisho, na ahadi za jinsi ya kutekeleza Mpango wa Mission 300.”amesema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko