The House of Favourite Newspapers
gunners X

Dkt. Mpango: Siogopi Vitisho, Makontena ya Makonda Yapigwe Mnada

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameagiza makontena 20 ya samani yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,  na bado yapo bandarini baada ya kushindwa kuyalipia kodi, yapigwe mnada na kwamba hajali vitisho vya mwanasiasa huyo kwani ameapa kusimamia sheria na kanuni za kodi zilizopo nchini.

 

Mpango ametoa maamuzi hayo leo Jumatatu, Agosti 27, 2018 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) alipofanya ziara ya kushtukiza na kukagua makontena hayo katika Bandari Kavu ya Dar es Salaam (DICD).

 

“Sheria za nchi hazichagua sura wala cheo cha mtu, na mimi ndicho nilicho apa, kutekeleza sheria za nchi, sheria za kodi, ndiyo dhamana niliyo pewa kwahiyo Kamishna, simamia sheria za kodi bila kuyumba” alisisitiza Dkt. Mpango akitoa maelekezo kwa Kamisha wa Forodha, Bw. Ben Usaje.

Alifafanua kuwa mzigo wa Samani ulioagizwa kutoka nje ya nchi hauna msamaha wa kodi na kwamba huyo aliye agiza (RC Paul Makonda) alipe kodi stahidi na asipo lipa kodi hiyo mchakato unaoendelea wa kuyapiga mnada makontena hayo uendelee.

“Napenda niwaombe viongozi wenzangu Serikalini, ni muhimu tukachuja maneno! Unasema mtu anayekuja kununua samani atapata laana, tena laana ya Mungu, kwanini tunamhusisha Mungu kwenye vitu vya namna hii” alieleza kwa masikitiko Dkt. Mpango

Dkt. Mpango alitoa wito kwa watanzania wanaotaka kununua bidhaa hizo ambazo nyingi ni vifaa vinavyoweza kutumika shuleni ama maofisini kama vile viti meza na makabati, kujitokeza bila hofu kununua mali hizo.

Aliwaomba walimu na wanafunzi wasiwe na wasiwasi na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua na kuwekeza kwenye elimu kwa kutenga zaidi ya shilingi bilioni 20 kila mwezi kulipa ada ya wanafunzi ili wasome bila kulipa ada na ina mpango madhubuti wa kuboresha miundombinu ya elimu nchi nzima ikiwemo ujenzi wa madarasa na ofisi za walimu.

“Tunawapenda na kuwathamini sana walimu wetu, asitokee mtu yeyote akaanza kuwaambia hadithi kama vile Serikali hii inawapuuza! Si kweli hata kidogo” Aliongeza Dkt. Mpango

Kwa upande wake, Kamishna wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Ben Usaje, alimweleza Dkt. Philip Mpango kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda, aliwasilisha maombi ya kutaka kupewa msamaha wa kodi wa makontena 36 yenye samani kutoka Diaspora nchini Marekani.

Alisema kuwa kati ya makontena hayo, yaliyoingia nchini ni makontena 20 ambayo yanadaiwa kodi ya shilingi bilioni 1.2 na kwamba utaratibu kwa kumtaka Paul Makonda alipe kodi hiyo ili aruhusiwe kuyachukua makontena hayo ulifanyika kwa mujibu wa sheria na kwamba mpaka sasa hajayachukua ndio maana yanapigwa mnada.

Naye aliwatahadharisha watu wanao tumia masuala ya siasa na uongozi Serikalini kutaka kukwepa kulipa kodi a kwamba suala la kodi za samani zinaonekana ziko juu kwa sababu Bunge lilitunga sheria hiyo ili kulinda soko la ndani la samani na kuweka sheria ya kutokuwepo kwa msamaha wowote wa kodi kwenye bidhaa kama hizo.

 

Maamuzi hayo ya Dkt. Mpango yamekuja ikiwa ni siku mbili baada ya TRA kuyapiga mnada makontena 20 yaliyoingizwa nchini kwa jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,  ambapo mkuu huyo jana alifanya ibada ya kumuomba Mungu yasipate wateja.

 

 

Makonda alishiriki ibada ya pili katika Kanisa la Anglikana, iliyoongozwa na Mchungaji Sabimbona Rushashi, mjini Ngara mkoani Kagera.

 

Akizungumza akiwa wilayani Ngara kwenye msiba wa mama mkubwa wa mke wake, alisema sababu za kumfanya afanye ibada hiyo ni kuumizwa na kitendo hicho kilichofanywa na TRA wakati ikitambua makontena hayo si mali zake binafsi.

 

Alisema pia katika ibada hiyo, amewaombea walimu na wanafunzi wa mkoa huo na wananchi ambao wamejitolea kuchangia juhudi hizo za kujenga ofisi za walimu wasivunjike moyo.

 

“Amelaaniwa mtu yule atakayenunua furniture (samani) za walimu. Nimefanya ibada maalumu leo (jana) ya kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa sababu naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaofanya kazi katika mazingira magumu ikiwa ni jitihada zangu binafsi,” alisema Makonda.

 

Juzi kontena moja la samani hizo lilikuwa  likiuzwa kwa Sh. milioni 60 wakati wateja waliofika kununua walifikia gharama ya Sh. milioni 30.

Kontena hizo ambazo zilipigwa mnada na kampuni ya udalali ya Yono Action Mart, zilikuwa na samani aina ya meza, viti na mbao za kufundishia wanafunzi.

Kontena hizo zinapigwa mnada kutokana na kushindwa kulipiwa kodi ya Sh. bilioni 1.2 zinazodaiwa na TRA baada ya kuwasili nchini.

 

Sakata Lilipoanzia

Habari za kuwapo kontena hizo zilitolewa tangazo la TRA la kuwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia na kuondoa mizigo yao, huku ikitishia kuzipiga mnada iwapo hawatatokea ndani ya siku 30.

 

Mei 12, mwaka huu, Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye, alisema wamiliki wa mizigo hiyo wanatakiwa kuikomboa ndani ya siku 30 kuanzia siku hiyo.

Katika tangazo hilo lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News, pia lilikuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800.

 

Aidha, barua ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza kuwapo kwa ombi la msamaha wa kodi wa mali hizo, maombi ambayo hayastahili kuridhiwa, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi.

 

Kadhalika, barua hiyo ambayo haikuthibitishwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) wala Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, iliandikwa na mamlaka hiyo ya ukusanyaji kodi kumueleza waziri husika kuwa ombi hilo haliwezekani kwa kuwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa haina sifa ya kupata msamaha kwa mujibu wa sheria.

Comments are closed.