Dkt. Nchimbi Aagiza Pembejeo za Kilimo Zipelekwe Mtwara Kwa Wakati
Katibu Mkuu wa Chama hicho,Balozi Dkt,Emmanuel Nchimbi ametoa maagizo mbalimbali kwa serikali ikiwemo kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa bei nafuu na kwa wakati.
Maagizo hayo ameyatoa jana wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho na wananchi katika uwanja wa sabasaba mkoani Mtwara.
Amesema kwa miaka michache Wanamtwara wamepiga hatua katika kilimo ambapo kuna kila dalili zinazoonyesha habari za umaskini zitabaki hadithi katika mkoa wa mtwara.
“Naiagiza serikali ihakikishe pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu,mikoa ya Kusini malalamiko ni mengi kuhusu jambo hilo. Hata masoko yapatikane”amesema
Dk. Nchimbi amesema serikali imetenga Sh.bilioni 150 kwa ajili ya upanuzi wa Bandari ya Mtwara.
Amesema tangu serikali iwekeze nguvu katika uendelezaji wa bandari hiyo matokeo chanya yameanza kuonekana ikiwemo ongezeko la mapato ya Sh.bilioni 25.
”Maelfu ya tani yanasafirishwa na kuletwa mkoani mtwara kupitia bandari hiyo, sasa hivi utegemezi wa bandari ya Dar es Salaam umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na uboreshwaji wa bandari hii ya Mtwara,”
”Natoa wito kwa Serikali kuendelea kuimarisha bandari hii ambayo ni mkombozi wa mikoa ya kusini hii iwe tegemeo katika mikoa yetu na kuendelea kupunguza msongamano katika bandari ya Dar es Salaam na kufanya bidhaa zitoke kwa wakati na kuwafikia walengwa,”amesema.