Dkt. Philip Mpango: Serikali Itaendelea Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwemo kuimarisha hali ya ulinzi, amani na usalama na kuboresha mfumo wa viwango vya kodi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Kodi na Uwekezaji la Mwaka 2025 linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Ametoa rai kwa washiriki wa Kongamano hilo kujielekeza katika kuibua mawazo na mikakati mipya itakayowezesha Taifa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani na hivyo kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi na kupunguza utegemezi kwa wahisani.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kutumia vema fursa inayotolewa na Serikali kila mwaka kutoa maoni na kuwasilisha mapendekezo yao ya kuboresha sera za kodi na uwekezaji kwa kuchangia moja kwa moja katika jukwaa hilo au kupitia dirisha la kidigitali.
Pia amewaagiza Mawaziri wa kila sekta kutoa maoni ya kuongeza mapato ya ndani katika sekta zao na kuhakikisha kuwa maoni na mapendekezo yatakayotolewa na wadau kwa njia mbalimbali yanafanyiwa kazi bila kudumaza ukuaji wa sekta husika.
Makamu wa Rais amesema zipo hatua mbalimbali zinazopaswa kutekelezwa zinazoweza kuongeza mapato ya ndani ikiwemo kuweka mkazo zaidi katika kuimarisha uwezo wa ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya ndani, kuongeza jitihada katika kuboresha mfumo wa kodi ambao utahakikisha usawa na kuondokana na misamaha ya kodi isiyo na tija pamoja na kutoa vivutio vya kutosha kwa mawakala na taasisi za kukusanya kodi na kukabiliana na vitendo vya rushwa.