The House of Favourite Newspapers

DNA Yamuumbua Aliyetelekeza Watoto Wawili, Atupwa Jela!

DNA (Kipimo cha Vinasaba) ni noma kwani kinawatoa kijasho wengi! Kwa muda mrefu kumekuwa na vilio vya baadhi ya wanawake wanaolia kutelekezewa watoto bila kujua kwamba kuna sheria ya kuwashikisha adabu wanaume wenye tabia hiyo hasa wale wanaogoma kwenda kupima DNA.

 

Tukio la mfano ni la mfanyabiashara mwenye jina kubwa mjini Morogoro, Hamis Rajab Bilal ambaye Ijumaa iliyopita alihukumiwa kifungo cha kwenda jela miezi mitatu na kulipa faini ya shilingi laki tano baada ya kukutwa na hatia katika Mahakama ya Mwanzo iliyopo Nunge kwa kosa la kutelekeza watoto wake wawili aliozaa nje ya ndoa.

 

Hukumu hiyo iliyovuta hisia za wengi ilitolewa na hakimu wa mahakama hiyo, Emilia Hamis Mwambusi ambaye alisema alitoa adhabu hiyo kali ili iwe fundisho kwa baadhi ya wanaume wanaozaa nje ya ndoa na kutelekeza watoto wao.

 

Awali, akisoma hukumu hiyo ya kesi namba 73 ya Mwaka 2018, hakimu huyo alisema kwamba, mahakama hiyo ilimtia hatiani Hamis baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mlalamikaji, Mwajuma Said aliyewasilisha mahakamani hapo vyeti vya kuzaliwa vya watoto hao vyenye ubini wa jina la mlalamikiwa.

 

 

Akiendelea kusoma huku hiyo, Mwambusi alisema kuwa, kitendo cha Hamis kuikatalia mahakama kupima DNA kilisababisha mahakama hiyo kuamini kwamba watoto hao ni wake, licha ya mtuhumiwa huyo kuwakana kwamba siyo wake.

Baada ya kusoma hukumu hiyo iliyochukua takribani saa moja na nusu, Hakimu Mwambusi alitaja vifungu vilivyomtia hatiani Hamis kuwa ni kifungu namba 134, na tafasiri ya sheria ya mtoto sura ya 13.

 

“Wewe unajua una ndoa yako, unachepuka hadi unazaa nje ya ndoa kisha unawakana watoto wako, hutoi matunzo, hali hii inasababisha watoto kukosa haki ya msingi ya chakula, afya na elimu na kusababaisha ongezeko la watoto wa mtaani au Panya Road.

“Baada ya mahakama kukutia hatiani, ili iwe fundisho kwa wanaume wengine wenye tabia kama hizi, mahakama inakupa adhabu mbili.

 

“Kwanza utatumikia kifungo cha miezi mitatu jela. Pili utalipa faini ya shilingi laki tano na mwisho ukimaliza adhabu hizo, utawajibika kuwatunza watoto hawa mpaka watakapojitegemea,’’ Hakimu Mwambusi alimweleza Hamis wakati akimsomea hukumu hiyo.

Baadhi ya watu waliofurika mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo waliipongeza mahakama kwa kutoa adhabu hiyo.

 

Katika hatua nyingine, wakati mfanyabiashara huyo akipanda difenda kuelekea gerezani kwenda kuanza maisha mapya, alimtolea maneno ya vitisho mwandishi wetu aliyekuwa akimpiga picha.

STORI: Dunstan Shekidele, Morogoro

Comments are closed.