The House of Favourite Newspapers
gunners X

Dogo Janja Afichua Mapya Kuhusu Irene Uwoya “Tulifunga Ndoa Kweli, Tuliachana Vizuri”

0
Staa mkubwa wa muziki wa Kizazi Kipya nchini Tanzania, Dogo Janja au Janjaro.

 

DOGO JANJA au Janjaro; ni staa mkubwa wa muziki wa Kizazi Kipya nchini Tanzania ambaye aliingia kwenye sanaa kwa namna ya ajabu kabisa. Licha ya Arusha anakotoka kuwa na historia ya kutoa wanamuziki wengi, wazuri wa kitaifa na kimataifa, lakini aliibuliwa na kijana kutoka Manzese jijini Dar, Madee.

 

Madee alikuwa katika ziara ya kawaida ya kimuziki jijini Arusha miaka kadhaa iliyopita, lakini akashangazwa na kipaji cha msanii huyo ambaye kimsingi, alipaswa kuwa darasani shule ya msingi akisoma.

Madee alipomchukua Dogo Janja na kutinga naye jijini Dar na kumpa nafasi ya kuonesha kipaji chake, kweli kijana huyo wa Arachuga akaonesha umahiri mkubwa na kila mmoja akamkubali. Dogo Janja ameingia kwenye gemu kirahisi sana katika umri wake mdogo.

Dogo Janja akiwa na aliyekuwa mke wake, Irene Uwoya.

Ndani ya Lebo ya TipTop Connection, Dogo Janja alikuwa ndiye msanii mdogo kuliko wote na kazi ambayo aliifanya ilionesha ubora wa hali ya juu kiasi cha kugeuka lulu.

 

Kuna wakati, baadhi ya watu wakaanza maneno ya kumsema Madee kuwa alikuwa akimtumia dogo huyo kupiga hela. Walikuwepo hadi watu waliomfuata Dogo Janja mwenyewe na kumweleza kuwa ananyonywa, kiasi kilichomfanya Dogo Janja atangaze kujitoa kwenye kundi hilo, tena huku akitoa maneno mabaya kwa Madee, akisema anafanya shoo nyingi lakini hapewi hela.

Watu wengi walikuwa upande wake alipotangaza kuondoka, wakiamini alipaswa kufaidika kwa kipaji chake. Ni kitu cha kawaida katika kazi yoyote, changamoto ni nyingi katika maisha hivyo halikuwa jambo la ajabu baada ya kujifunza, akarejea tena TipTop Connection na kuendelea na mzigo. Sasa; katika umri wake mdogo, Dogo Janja aliwahi kudaiwa kufunga ndoa na supastaa wa filamu nchini Tanzania, Irene Uwoya.

 

Hata hivyo, baada ya kupita kipindi kirefu, Dogo Janja ambaye jina lake halisi ni Abdulaziz Abubakar amefichua kile kile kilichotokea kati yake na Uwoya mwaka 2017.

Dogo Janja akiwa na mpenzi wake wa sasa.

Katika maisha yao ya kupendana na Uwoya, Dogo Janja alifunga ndoa yenye utata na mwanamama huyo hivyo wengi kuona kama ilikuwa ni maigizo; Katika mahojiano maalum (exclusive) na mwandishi wetu, Dogo Janja anafunguka mengi kama ifuatavyo;

IJUMAA SHOWBIZ: Hebu tueleze ukweli kuhusu ndoa yako na Uwoya, ilikuwa ndoa ya kweli au maigizo?

DOGO JANJA: Ile ilikuwa ndoa ya kweli na nikiri tu kwamba hatukuwashirikisha wazazi.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa nini kitu kikubwa kama hicho msishirikishe wazazi?

DOGO JANJA: Kwa kweli tulifanya makosa, lakini kifupi tu mimi nasema mapenzi ni upofu, naukubali usemi huo.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, au ni kama watu wanavyosema kwamba ulilogwa?

DOGO JANJA: Kwa kweli sisi kama mastaa hatuamini uchawi; ni mapenzi tu yalitufunika usoni.

IJUMAA SHOWBIZ: Wewe ullelewa kimuziki na msanii maarufu Madee, je, naye hukumshirikisha katika hili la ndoa na Uwoya?

DOGO JANJA: Kwa kweli sikumshirikisha na yeye alidhani ni muvi, alijua ni muvi.

IJUMAA SHOWBIZ: Je, mliachana baada ya kugombana? Na je, mligombea nini?

DOGO JANJA: Hapana; hatukugombana, tulikubaliana tu kwamba hii miaka mitano inatosha, hatukuachana vibaya. Hutakiwi kuachana vibaya na x-wako; hujui nani atakuokota siku moja ukianguka.

IJUMAA SHOWBIZ: Unawashauri nini vijana kuhusu kuwa na wapenzi na kupendana?

DOGO JANJA: Nasema tu kwamba kiukweli mapenzi ya vijana hayadumu kwa sababu wanabanana sana na wengine inatokea mpenzi wako hakuheshimu ipasavyo hivyo pendo linakwisha ghafla.

IJUMAA SHOWBIZ: Nini kinatakiwa kwa vijana ili penzi lao liweze kudumu?

DOGO JANJA: Njia ni moja tu; ni kwamba inatakiwa uaminifu kwa sababu hata mgombane vipi kama ni mkeo mtalala kitanda kimoja na kujifunika shuka moja.

IJUMAA SHOWBIZ: Ikitokea mwanamke ndiye mgomvi na siyo wewe mwanaume, unawashuri wafanye nini vijana wanaokumbwa na hilo?

DOGO JANJA: Ikitokea mwanamke akawa mgomvi ni bora wewe mwanaume ukawa mkimya na kama anazidi kukukosesha raha ni bora uondoke hapo kuepusha shari.

IJUMAA SHOWBIZ: Ukiondoka hapo alipo mwanamke wako huyo mkorofi utakuwa umetatua jambo?

DOGO JANJA: Kwanza kabisa ni vema kumjua mwanamke wako kisaikolojia, kuna lugha ya kuongea naye utakaporudi. Mjue sana mwenzako, utaepusha mambo mabaya kutokea kati yako na yeye. Mwanamke akikuudhi sana ni bora kumuacha salama.

IJUMAA SHOWBIZ: Unawashauri nini vijana wa siku hizi ambao wanakusoma?

DOGO JANJA: Nawashauri bora sasa watafute fedha kwa sababu ni kweli kwamba wengi wanaumizwa sana na wanawake.

IJUMAA SHOWBIZ: Nasikia una mpenzi mpya, ulimpataje huyo?

DOGO JANJA: Ni kwamba nilikuwa frustrated baada ya kuvunjika ndoa yangu ya kwanza nikampata mtu wangu wa sasa baada ya kuchati naye; ni malaika na sasa ninavyozungumza yupo Zanzibar, ni vigumu sana kumzoea kwa kuwa yeye yupo Zanzibar, lakini nina amani sana moyoni.

IJUMAA SHOWBIZ: Asante sana.

DOGO JANJA: Poa.

Dogo Janja amezaliwa Septemba 15, 1994 pale Ngarenaro jijini Arusha. Kazi yake ya kwanza ya muziki ilianza kutoka mwaka 2016 akiwa ni mwanafamilia wa Tip Top Connection Group ya Babu Tale na Mdee.

Miongoni mwa ngoma zake zilizotisha ni pamoja na My Life aliyoipakua mwaka 2016 na mwaka 2017 akamuoa Uwoya ambaye amezaliwa Desemba 18, 1988. Uwoya alianza kuigiza mwaka 2007 na waigizaji hodari wakiwemo Vincent Kigosi almaarufu Ray na Steven Kanumba (marehemu).

Baadhi ya ngoma alizotoa na mwaka kwenye mabano ni ( 2016) My life, (2017) Ngarenaro, (2017) Ukivaaje Unapendeza, (2018) Banana, (2018) Mikogo Sio, (2018),  Wayu Wayu, (2018) Since Day One, (2019) Yente, (2020) Asante aliyomshirikisha Lady Jaydee na nyingine kibao.

DAVIDO APATA PIGO ZITO, MWANAYE AFARIKI AKIOGELEA KWENYE BWAWA, NI YULE ALIYEZAA NA CHIOMA..

Leave A Reply