The House of Favourite Newspapers

Domokaya Afunguka Kilichowapoteza, Aanika Mikakati Mipya

0

MPENDWA msomaji wa kolamu hii ya Yuko Wapi, leo nimekuletea mwanamuziki wa kizazi kipya; Precious Juma Mkona almaarufu kama Domokaya ambaye miaka ya 2003 waliunda kundi la pamoja na mwenzake Mandojo, ambao walitikisa kwa kipindi hicho.

 

Kundi hilo la watu wawili lilijipatia umaarufu mkubwa na ngoma mbalimbali kama vile Wanoknok, Nikupe Nini, Nizikwe Hai, Niaje, Dingi, Wapambe, Nenda na nyingine nyingi zikiwemo walizowashirikisha wasanii wengine.

 

Kundi hili la mtu mbili licha ya uwezo wao mkubwa, lakini waliweza kuwashirikisha wasanii wengine kwenye kazi zao kama vile; Juma Nature, Lady Jaydee, Mangwea na wengineo.

Mwanahabari wetu hivi juzi kati alibambana na Domokaya kwenye viunga vya Mlimani City Dar ambapo mahojiano yalianza kama ifuatavyo:

 

Risasi: Domokaya umepotea sana kwenye gemu, vipi kaka?

Domokaya: Nipo kaka mitkasi tu.

Risasi: Mashabiki wenu wangependa kujua kama kundi lenu la Mandojo na Domokaya bado lipo hai au ndiyo lishasambaratika.

Domokaya: Hilo siwezi kuliweka wazi mimi kwa maana nisije nikakwambia lipo, alafu mwenzangu akasema vingine.

Risasi: Lakini kwa majibu hayo, inaonekana kuna sintofahamu. Vipi kwa upande wako maskani bado Arusha lilipoanzia kundi lenu?

Domokaya: Arusha kweli ndipo lilipoanzia kundi letu, lakini baadaye muziki ukatuhamishia Dar na mpaka sasa wote makazi yetu ni Dar.

Risasi: Ukiachana na muziki, unapiga dili gani zingine za kukuingizia kipato?

Domokaya: Ukiachana na muziki, nafanya biashara za hapa na pale.

Risasi: Kama zipi hizo, pengine mashabiki wako wangependa kuja kuendelea kukuunga mkono.

Domokaya: Ni biashara mbalimbali sina biashara moja.

Risasi: Vipi kuhusu familia?

Domokaya: Nina familia ya mke na mtoto mmoja wa kiume ambaye mwezi ujao Mungu akipenda, anatimiza miaka 11.

Risasi: Vipi harakati za kimuziki ndiyo umeshaachana nazo?

Domokaya: Siwezi kuachana na harakati za kimuziki kwa kuwa tayari muziki uko kwenye damu, hivi tunavyoongea nimeshaandaa kazi zangu za maana ambazo natarajia kuibuka nazo hivi karibuni.

Risasi: Hivi ni nini kiliwafanya mpotee kwenye gemu?

Domokaya: Ukweli kilichotufelisha ilikuwa ni menejimenti, kipindi chetu hatukuwa na menejimenti zenye nguvu kama walizonazo hawa madogo zetu wa sasa hivi kama kina Diamond, Harmonize na wengineo, ndiyo maana hatukuweza kutoboa kama wao.

Risasi: Sasa kama mkongwe, unawashauri nini hao madogo na wengineo?

Domokaya: Mimi nawashauri waache kuiga vionjo vya utamaduni wa nje kama vile Nigeria, Congo na kwingineko na waache kuimba matusi.

Risasi: Vipi ungependa mwanao awe mwanamuziki kama wewe?

Domokaya: Mwanangu siwezi kumchagulia kazi, nitamuacha achague kazi anayoipenda. Siwezi kumfanyia kama tulivyofanyiwa sisi kipindi hicho tulipokuwa tukijifunza muziki, tulikuwa tukionekana kama tumepinda.

Risasi: Asante Domokaya nakutakia kazi njema.

Domokaya: Asante.

Leave A Reply