The House of Favourite Newspapers

Donald Ngoma atoweka Yanga

0

Donald-Ngoma-1 Donald Ngoma.

Martha Mboma, Dar es Salaam
WAKATI kikosi cha Yanga kikianza mazoezi rasmi jana Alhamisi kikiwa na wachezaji sita, mshambuliaji wa timu hiyo, Mzimbabwe, Donald Ngoma ameshindwa kuungana na timu hiyo kwa wakati huku kukiwa na taarifa tata juu ya kutokuwepo kwake mazoezini.

Yanga wameanza mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini jijini Dar huku wachezaji sita wakihudhuria mazoezi hayo, ambao ni Thaban Kamusoko, Godfrey Mwashiuya, Pato Ngonyani, Benedict Tinoko, Oscar Joshua na Deogratius Munishi ‘Dida’.

Awali, kulikuwa na taarifa kuwa Ngoma ambaye naye alitakiwa kuwepo katika mazoezi hayo kutokana na kutokuwa na majukumu ya timu ya taifa, ameshindwa kufika nchini na kujiunga na wenzake kutokana na kufiwa na mjomba wa mke wake hukohuko Zimbabwe.

Akizungumza na Championi Ijumaa, mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano cha timu hiyo, Jerry Muro, alisema Ngoma hajafika nchini lakini taarifa za kufiwa wao pia hawajazipata rasmi.

“Siwezi kulitolea ufafanuzi suala lake hilo la kufiwa kwa sababu taarifa tunapata kupitia vyanzo tofauti,” alisema Muro.

Kwa upande wa meneja wa timu hiyo, Hafidhi Salehe, alipopigiwa simu na kuulizwa juu ya suala hilo la wachezaji wa kimataifa ambao hawana majukumu ya timu za taifa, alisema: “Wote wapo na tunaendelea na mazoezi hivi sasa.”

Wachezaji ambao hawakuhudhuria mazoezini lakini walitakiwa kuwepo ni; Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Deus Kaseke na Andrey Coutinho.

Leave A Reply