The House of Favourite Newspapers

Donald Trump Akabiliwa na Mashtaka Saba Uhifadhi wa Nyaraka za Siri

0

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ameshtakiwa kwa kushughulikia nyaraka za siri baada ya kuondoka Ikulu ya White House.

Bw Trump, 76, anakabiliwa na mashtaka saba ikiwa ni pamoja na kuhifadhi faili za siri zilizoainishwa bila kibali, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti. Hadi kufikia sasa mashtaka bado hayajaonekana hadharani.

Ni shitaka la pili dhidi ya Trump na shtaka la kwanza kabisa la kutoka upande wa serikali kwa rais wa zamani.

Trump amekuwa akifanya kampeni ya kurudi Ikulu mnamo 2024.

Katika chapisho kwenye mtandao wa Truth Social,  Trump alisema hakuwa na hatia na ametakiwa kufika katika mahakama mjini Miami Jumanne alasiri, ambapo atakamatwa na kusikiliza mashtaka dhidi yake.

“Sikuwahi kufikiria kuwa jambo kama hilo linaweza kumpata rais wa zamani wa Marekani,” aliandika.

Aliongeza: “Kwa hakika hii ni siku ya giza kwa nchi ya Marekani, lakini kwa pamoja tutaifanya Marekani kuwa Kuu tena!”

Wakili wa  Trump Jim Trusty aliambia shirika la habari la CNN kuwa rais huyo wa zamani alikuwa amepokea maelezo ya mashtaka katika hati ya wito.

Alisema ni pamoja na kula njama, taarifa za uongo, kuzuia haki, na kuhifadhi nyaraka za siri kinyume cha sheria chini ya Sheria ya Ujasusi.

Idara ya Haki (DOJ) ilikataa kutoa maoni na hati ya mashtaka haijatolewa hadharani.

Hati ya mashitaka ni hati inayoweka wazi maelezo ya mashtaka dhidi ya mtu, kuhakikisha kuwa ana taarifa ya makosa ya jinai yanayodaiwa.

Wakati huo huo, maofisa wa ujasusi wa siri watakutana na wasimamizi wa sheria ili kupanga safari ya Bw Trump hadi mahakama ya Miami katika siku zijazo.

Mwendesha mashtaka maalum Jack Smith amekuwa akizingatia ushahidi katika kesi ya hati tangu alipoteuliwa kuisimamia na Mwanasheria Mkuu Merrick Garland mnamo Novemba.

Mwaka jana, nyumba ya kifahari yake Bw Trump iliyopo Florida Mar-a-Lago ilipekuliwa na hati 11,000 zilinaswa, zikiwemo takriban 100 zilizowekwa alama kama zilizoainishwa. Baadhi ya hizi zilikuwa na maandishi siri kuu.

Kulikuwa na ripoti wiki jana kwamba waendesha mashitaka walipata rekodi ya sauti ya Bw Trump ambapo alikiri kuhifadhi hati ya siri baada ya kuondoka Ikulu ya White House.

Ni kinyume cha sheria za Marekani kwa maafisa wa serikali – ikiwa ni pamoja na rais – kuondoa au kuweka hati zilizoainishwa katika eneo lisiloidhinishwa.

Wataalamu wa sheria walisema kufunguliwa mashtaka hakutazuia uwezo wa Bw Trump kuwania tena kiti cha urais.

“Anaweza kushtakiwa mara kadhaa na haitazuia uwezo wake wa kugombea nafasi,” anasema David Super, profesa katika Kituo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Georgetown.

Super alibainisha kuwa Bw Trump anaweza kuendelea kuwania wadhifa huo hata kama atapatikana na hatia katika kesi hiyo ya stakabadhi.

FEI TOTO AZUNGUMZA AKIWA AZAM – ”TAFANYA KAMA YANGA, TUTACHUKUA UBINGWA”…

Leave A Reply