The House of Favourite Newspapers

DONDOO MUHIMU ZA KUNOGESHA PENZI KWA WANANDOA

KWANZA namshukuru Mungu kwa kunijaalia afya njema na pia kwa kunipa nguvu ya kuandika hiki ninachokusudia. Ungana nami ili ujifunze kitu. 

 

Kwa wale wasiofahamu niwaambie tu kwamba dhana ya mapenzi ina wigo mpana sana na ndio maana hutasikia hata siku moja tumepumzika kuyazungumzia. Hata hivyo, tunachofanya siku zote ni kukumbushana kwa yale tunayoyafahamu na kushauriana pale tunapohisi wengi hukosea.

 

Kwenu ninyi mlio katika mapenzi, hasa wanandoa, kwanza yawapasa mfahamu kitu mapenzi ni tunu au zawadi maalum kutoka kwa mola wetu.

 

Mungu ametuwekea mapenzi ili tupate raha na amani katika maisha yetu, hivyo wanaoyachezea na kuyavuruga kwa makusudi kwa kuumiza hisia za wenzao na kuwasababishia simanzi, si watu wa kupendeza mbele ya macho ya wale wanaojua hasa nini maana ya mapenzi. Kwa kulifahamu hilo, naomba niwausie yafuatayo;

Kwenu wanaume; ninyi mnachukua nafasi ya baba yenu Adamu. Baba yetu Adamu alimpenda mke wake kwa dhati hata akashawishika kula tunda alilokatazwa ili mradi asimsononeshe mkewe. Yawapasa mfahamu kuwa wanawake ni zawadi kwenu, pumziko na tulizo la mioyo yenu. Wanawake ndio raha yenu na amani kubwa ya maisha yenu.

 

Kosa kubwa mnalofanya wanaume ni kuutumia vibaya mfumo dume hasa katika suala nyeti kama mapenzi. Mapenzi si ubabe, mapenzi ni upole na ukarimu. Pamoja na kwamba mmebarikiwa kwa kupewa nafasi ya kuwa kichwa katika nyumba lakini linapokuja suala la kurekebisha tofauti zinazojitokeza katika mahusiano yenu, si vyema kutumia njia za kibabe.

 

Niwaambie kitu, wanawake wana hisia sana na wamebarikiwa upendo wa hali ya juu, ndio maana wakapewa dhamana ya kubeba mtoto tumboni kwa miezi tisa na pia kumnyonyesha na kumlea kwa miaka kadhaa, wewe ungeweza?

 

Nasema ni watu wa hisia kwa sababu, hivi uliwahi kufikiri ni kwa nini wanawake huridhika sana na kujisikia poa kweli wanapopewa zawadi kama ya maua na kadi zenye ujumbe wa mapenzi ukilinganisha na wanaume? Unafikiri ni kwa nini wana machozi ya haraka wanapotendwa? Au unafikiri ni kwa nini wanapenda kutumiwa meseji za kimahaba ‘love message’ zaidi kuliko kupigiwa simu? Jiulize.

Mimi nawaona wanawake kama watu wa kuheshimiwa na kupendwa sana. Mkumbuke wanawake ndio mama zetu, walezi wetu na ndio nyumba zetu. Jaribuni pia kujicontrol na huo mnaouita ukijogoo kwamba eti ninyi ni watu msioridhika na mpenzi mmoja.

 

Jaribuni kuufuta usemi wa ‘Wanaume hawaaminiki hata kidogo’. Ridhika na mpenzi uliye naye, heshimu hisia zake na thamini mapenzi yake kwako na mpe ile kitu roho inapenda!

 

Kwenu wanawake; Kimaumbile wanaume wanapenda kuona wanasikilizwa na wake zao au wapenzi wao na hawakawii kubadilika wanapokwazwa. Pamoja na kwamba nanyi mna sauti ndio, lakini wanaume ni watu wa kuwasoma kwanza na kuwaendea taratibu kuliko kuwapandishia na kuonesha kushindikana nao.

Kama kweli unampenda basi muoneshe unamheshimu, hapo utampata! Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa makala nyingine bomba kabisa.

Comments are closed.