The House of Favourite Newspapers

DP: Mtikila aliawa kabla ya ajali

0

Christopher-MtikilaMarehemu Mch. Christopher Mtikila

Na Waandishi Wetu

MAPYAA! Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrati (DP), Abdul Juma Mluya ameibuka na kusema mazingira ya kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Mchungaji Christopher Mtikila yamejaa utata huku akiweka wazi kwamba, inavyoonekana aliuawa kabla ya ajali yenyewe.

Mtikila alifariki dunia katika ajali ya gari aina ya Toyota Corolla namba T189 ARG, Oktoba 4, 2015 iliyotokea kwenye Kijiji cha Msolwa, Bagamoyo, Pwani. Wengine watatu walijeruhiwa.

mtikila2Mti ambao gari liliugonga kwa juu kabla ya kupinduka.

Akizungumza na Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ofisi ndogo ya chama hicho nyumbani kwa marehemu, Mikocheni B jijini Dar, Mluya alisema hata watu waongee vipi, lakini uchunguzi wao umeonesha kwamba, kiongozi wao aliuawa tofauti na eneo la ajali na mwili kwenda kutupwa pale.

ROHO YAKE ILIWINDWA KWA SIKU 40

Mluya alisema: “Ndugu mwandishi, Mchungaji Mtikila kama kufa alikuwa afe muda mrefu sana pengine siku arobaini zilizopita (mpaka siku ya kifo cha kweli), kwa sababu amewindwa na watu ambao hatujajua lengo lao kubwa lilikuwa nini!

“Kila alikokwenda kwa shughuli za kichama kulikuwa na timu ya watu inayomfuatilia.”

mtikila4…Baada ya Kupinduka

MARA YA KWANZA

“Tarehe siikumbuki, lakini ni Septemba mwanzoni. Tulikuwa Bunda, Mara kwenye shughuli za chama, kuna watu ambao walikuwa hawaeleweki walitufuata mpaka hotelini.

“Baada ya kubaini hilo, nilimuuliza mwenyekiti kuhusu ratiba aliyokuwa nayo ya kuzungumza kwenye runinga ya Staa TV.

“Alinipa ratiba. Baada ya kumaliza kuzungumza, nilimwambia Bunda si mahali pa kulala hivyo nilimshauri aondoke, aende Mwanza. Na nilimwambia dereva wake aondoke bila kuaga.”

mtikila4 (2)WAKIWA NJIANI

“Lakini cha ajabu, wakiwa njiani wakielekea Mwanza kuna gari liliwafuata kwa nyuma kwa mwendo ambao waliutulia shaka. Dereva wa mwenyekiti alipokuwa akiongeza mwendo, naye anaongeza, akipunguza naye anapunguza.

“Ilibidi dereva amwambie mwenyekiti naye akamtaka dereva aongeze kasi hadi Mwanza.”

“Katika ratiba yetu tulitaka kufanya ziara za kichama kuanzia  Oktoba 18,  mwaka huu kwa kuanzia mkoa wa Kigoma na kwingineko. Pamoja na kufuatiliwa kote kule mwenyekiti hakuwa na roho ya uoga hata kidogo. Alimtanguliza sana Mungu.

“Kwa hiyo wasiwasi mkubwa wa kufuatiliwa na watu hao ulianza Mara na Mwanza kwa nyakati tofauti.

“Septemba 11, mwaka huu ndiyo tarehe ambayo sasa nilianza kukariri matukio hayo hatua kwa hatua. Siku hiyo tulikwenda kwenye Kijiji cha Usangu mkoani Pwani kwa ajili ya kufanya kampeni ya mgombea udiwani. Baada ya kumaliza tuliamua kurudi Dar lakini njiani dereva akasema kuna watu hawajui wanakuja nyuma yetu.”

WAPOTEA NJIA KWA KUFUATILIWA

“Tulijikuta tukipotea njia na kutokea mjini Kisarawe (Pwani). Pale tulifika kituo cha mafuta ambapo tulikuta gari aina Toyota Land Cruiser VX limepaki kama vile ni watu pia walikuwa wakitufuatilia.

“Lengo la kusimama pale lilikuwa kupata chakula lakini hatukufanya hivyo kulingana na mazingira. Tukaanza safari ya kurudi Dar. Tulipofika Pugu Sekondari, gari lile lilitupita kwa kasi na kupotea.

“Tulipofika Tazara gari lile lilionekana na wakati huo yalikuwa mawili. Kilichotushangaza ni upya wa magari lakini eti namba zinaanzia na A. Mimi nilifikiria kwamba, pengine ni za idara  ya  usalama  wa  taifa  zilikuwa doria  mbalimbali hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

“Ndugu mwandishi, mimi ninafanya kazi ya siasa, niko makini sana. Niliwaambia wenzangu kuwa tunafuatiliwa.

“Ndani ya gari sisi tulikuwa na viongozi wa kuwapeleka Temeke. Lakini baada ya kufika huko lile VX tulikutana nalo. Tulipomuacha yule tuliyempeleka kule, tukawa tunampeleka mchungaji nyumbani kwake (Mikocheni) lakini bado lile gari lilikuwa likitufuatilia.”

WAPIGA CHENGA

“Tulipofika maeneo ya Msasani kwa Mwalimu (Julius Nyerere) dereva alikunja kona kuelekea kwa mchungaji na lile gari likakunja kona na kurudi lilikotoka.”

SIKU NYINGINE

“Siku iliyofuata tulipanga mipango yote ambapo sasa tulisema Oktoba 18, mwezi huu tuanze ziara ya mkoa wa Kigoma  na maeneo  mengine ya Kanda ya Ziwa.

“Mimi niliondoka kuelekea Shinyanga, yeye (Mchungaji) aliandaa safari ya kwenda Njombe kwenye kampeni ya mgombea Ubunge Jimbo la Njombe.”

OKTOBA 2, 3, 2015

“Mwenyekiti aliondoka Dar Oktoba 2, kuelekea Njombe. Oktoba 3, alinipigia simu asubuhi na kunijulisha kuwa  jana yake walipata ajali maeneo ya Makambako wakati wanakwenda.

“Nilimuuliza alipata matibabu, akajibu kuna viongozi wa Njombe walifika na kumchukua hivyo yuko sawasawa.”

TAARIFA YA AJALI

“Siku hiyo hiyo walifanya kampeni na jioni yake walianza safari ya kurejea Dar. Walipofika Mkoa wa Pwani, saa kumi na moja alfajiri, Mchungaji Mgaya alinipigia simu na kuniambia walikuwa njiani wanarudi Dar, wamepata ajali mbaya sana. Lakini hakuniambia kama mchungaji amefariki dunia.

“Nilianza kufuatilia tukio hilo na kuuliza kama kuna msaada wowote wameupata, akasema mpaka muda huo polisi walikuwa hawajafika. Mimi napenda sana kufungua mitandao ya kijamii, nilipofungua nikakuta picha zilishasambaa kwenye mitandao kitu ambacho nilijiuliza usiku huo huyo mpigapicha alikuwa wapi?”

SHAKA KUBWA YA DP

“Sisi DP, mashaka yetu makubwa ni mazingira mazima ya namna kiongozi huyo alivyofariki dunia. Hata mtoto hawezi kudanganywa kwa namna hiyo. DP ina taasisi ya kufanya uchunguzi iitwayo Liberty International Foundation iliyokuwa ikisimamiwa na marehemu. Ipo kazini kwa sasa ili kubaini ukweli wa kifo cha mwenyekiti na tutaweka wazi kila kitu.”

“Laini pia tunaitaka serikali kufanya uchunguzi na kutoa taarifa hadharani.”

MWENYEKITI KIJIJI AIBUKA NA YAKE

Uwazi pia lilifika aneo la ajali na kujionea kwa macho mazingira yake na kupata maelezo kutoka kwa baadhi ya mashuhuda.

Joshua Mohamed Msigala ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Msolwa, Chalinze, Pwani palipotokea ajali. Yeye anasimulia mambo aliyoelezwa na mmoja wa majeruhi, Mchungaji Patrick Mgaya siku ya tukio.

“Kwanza kabisa waandishi wa habari mmefanya vizuri kufika eneo la tukio na kujionea hali halisi. Nawaeleza hali halisi ilivyokuwa mpaka mimi kufika eneo la ajali.

“Siku hiyo asubuhi ya saa kumi na moja na nusu kama sikosei, nikiwa nyumbani nilipigiwa simu na dereva mmoja wa lori anayenijua. Akasema ameona ajali maeneo yangu lakini hajui kama kuna waliokufa au la!”

MWENYEKITI AWAHI NA BODABODA

“Kusikia hivyo, nilichukua bodaboda ili niwahi. Nilifika ndani ya dakika kama kumi tangu kutokea kwa ajali. Nilikuta mwili wa Mtikila umelala pembeni ya gari huku wengine watatu waliodai walikuwa ndani ya gari wakiwa wamesimama tu.

“Ila kati ya hao watatu, mmoja alijitambulisha kuwa ni Mchungaji Mgaya, yeye wakati nafika alikuwa akiongea kwa simu.”

ALICHOAMBIWA NA MCHUNGAJI

“Nilimuuliza mchungaji ilikuwaje? Akasema wakati wanapata ajali hiyo, marehemu Mtikila na wengine wawili walichomoka ndani ya gari hali iliyosababisha kifo cha Mtikila. Hata hivyo, kwa upande wangu sikuamini kama wote walichomoka kutoka kwenye gari bali mazingira yalionesha walitoka wenyewe.

“Mchungaji alizidi kuniambia kuwa, gari lilipaa juu zaidi ya futi kumi na kugonga mti kisha likapinduka na kulalia paa (kwenye Uwazi siku ya tukio, mchungaji alisema gari lilibiringika).

“Lakini pia siamini, kwani pamoja na kuona alama katika mti sikubali kama zilisababishwa na ajali kwani kama ni hivyo gari lingekuwa limepondeka zaidi juu lilikoangukia tofauti na lilivyokuwa likionekana.”

KILICHOMSHANGAZA ZAIDI MWENYEKITI

Mwenyekiti huyo alizidi kusimulia kushangaa kwake: “Kitu kingine kinachonishangaza ni kwamba, kwa maelezo yao gari liliacha barabara likawa linaendeshwa pembeni kwa umbali wa meta mia moja (urefu wa uwanja wa mpira). Kwa nini dereva asipunguze mwendo ambapo angefanya hivyo gari lisingefika kwenye mti.”

“Kinachoshangaza kingine ni kwamba, hakuna majeraha yaliyoonekana kwa macho kwa walionusurika hata kuonesha kwamba walikatwa na vioo wakati wakirushwa nje kutoka ndani ya gari. Hata viti vya mbele vilikuwa vilevile, havikuharibika na kama majeruhi walirushwa nje walipitia wapi?”

WALIOFIKA AWALI

Mwenyekiti huyo alisema anawashukuru askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wa Kambi ya Kizuka na Sangasanga waliokuwa wakipita ambapo walifika kutoa msaada.

“Baadaye mimi nilifanya mawasiliano na Polisi wa Kituo cha Chalinze (Bagamoyo) ambapo walifika eneo la tukio. Pia polisi wa mkoa nao walifika na saa 12:30 asubuhi majeruhi na mwili wa marehemu walipelekwa Hospitali Teule ya Rufaa Tumbi.”

Naye Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Msolwa, Joseph Hamad kwa upande wake alisema alipokea taarifa saa 3 asubuhi na alipowasiliana na mwenyekiti alimwambia yupo katika eneo la tukio.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliohojiwa na Uwazi walisema wameshangazwa na ajali hiyo iliyosababisha kifo cha Mchungaji Mtikila na kuitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina.

SIMU YA MTIKILA YAZUA UTATA

Mpaka tunakwenda mitamboni, familia ya Mtikila ilisema, jana ilitarajia kufuatilia simu ya marehemu kwani haijulikani ilipo na pia kujua walipo dereva (George Ponella) na msaidizi wake (Ally Mohamed) ambapo awali, dereva alishikiliwa na jeshi la polisi.

Habari imekusanywa na Makongoro Going, Haruni Sanchawa na Issa Mnali.

Leave A Reply