DRC Kuzungumza Na M23 Nchini Angola
Ofisi ya Rais wa Angola imetangaza kuwa itawasiliana na vuguvugu la M23 ili kundi hilo na serikali ya DRC wafanye mazungumzo ya moja kwa moja.
Tina Salama, msemaji wa Rais Félix Tshisekedi, hakuwa na uhakika kuhusu tangazo hilo lakini aliandika kwenye X kwamba Angola “itachukua hatua zinazohusiana na upatanisho”. Aliongeza kuwa serikali ya DRC inasubiri kuona utekelezaji wa mchakato huu wa upatanishi wa Angola.
Tangazo hilo limekuja baada ya ziara fupi ya Rais Tshisekedi nchini Angola, ambako alikutana na mwenyeji wake, Rais João Lourenço, kwa mazungumzo ya faragha.
Rais Lourenço, ambaye amekuwa mpatanishi wa mzozo wa DRC kwa takriban miaka minne, alitangaza mwezi uliopita kuwa atajiuzulu nafasi hiyo ili kuchukua wadhifa wa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.
Serikali ya DRC imekuwa ikikataa mazungumzo ya kikanda yaliyoitishwa na SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ajili ya kufanikisha mazungumzo na waasi wa M23. Hii imekwamisha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika vikao vya Luanda, Dar es Salaam, na Nairobi.
Awali, Rais Tshisekedi alisisitiza kuwa “maadamu mimi ni rais wa DR Congo” kamwe hatajadiliana na M23, akilitaja kundi hilo kama la kigaidi na kusema kuwa mazungumzo nao ni “mstari mwekundu ambao hatutavuka kamwe”. Hata hivyo, hatua yake ya kukubali mazungumzo sasa inaonekana kuwa muhimu katika juhudi za kurejesha amani kwenye eneo la Maziwa Makuu.
Wakati huo huo, SADC inatarajia kuitisha mkutano utakaohusisha serikali ya DRC na waasi wa M23 ili kutafuta suluhu ya kudumu kwa mzozo huo.
Serikali ya DRC pia inakabiliwa na lawama kutoka kwa Rwanda kwa kushindwa kutekeleza mazungumzo ya Luanda yanayohusu kuwaondoa wapiganaji wa FDLR, kundi linalopigana dhidi ya serikali ya Rwanda na ambalo linaendesha harakati zake ndani ya DRC.
Kwa upande wake, DRC imeendelea kuihusisha Rwanda na uungaji mkono wa M23, madai ambayo Rwanda imeendelea kukanusha.