The House of Favourite Newspapers

DRC yalaani mauaji ya raia 52 yaliyofanywa na M23

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imelaani mauaji ya raia 52 yaliyofanyika usiku wa Ijumaa hadi Jumamosi katika mji wa Goma wa mashariki mwa nchi hiyo ikisema kuwa, waasi wa M23 ndio waliofanya mauaji hayo ya umati.

Katika taarifa rasmi iliyotiwa saini na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani wa DRC, Jacquemain Shabani, serikali ya Kinshasa imewashutumu waasi wa M23 kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Mapigano makali yaliripotiwa kuzuka Ijumaa usiku katika sehemu ya magharibi mwa Goma, makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini huko mashariki mwa DRC. Hayo ni kwa mujibu wa duru nyingi za ndani ya Kongo.

Walioshuhudia tukio hilo kutoka vitongoji vya Keshero na Lac-Vert vya mji huo wamesema kwamba milio ya risasi na makombora ilianza kusikika yapata saa nne usiku Ijumaa na kusababisha hofu kubwa miongoni mwa wakazi wa mji huo. mapigano hayo yaliendelea hadi juzi Jumamosi asubuhi

Kwa mujibu wa vyombo kadhaa vya habari vya ndani, mapigano hayo yaliwahusisha waasi wa M23, ambao wameidhibiti Goma tangu Januari na wanamgambo wenye silaha wanaohusishwa na makundi yanayoshirikiana na Jeshi la Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaani (FARDC).

Taarifa iliyotangazwa na redio za eneo hilo imewanukuu waasi wa M23 wakidai kuwa muungano wa FARDC-Wazalendo ndio ulioanzisha mashambulizi hayo yaliyoendelea usiku kucha.

STORI: ELVAN STAMBULI