The House of Favourite Newspapers

Dully Atoboa Siri Kutozeeka!

HUYU jamaa hapendi kuitwa msanii, bali hupendelea kuitwa mburudishaji kwani asilimia kubwa ya ngoma zake ni za kucheza na siyo kusikiliza.

 

Stejini hujulikana kwa jina la Prince Dully Sykes au Dully, lakini jina alilopewa na wazazi wake ni Abdulwaheed Sykes.

Dully au Sauti ya Dhahabu ni mmoja wa wakongwe wa muziki huu wa Bongo Fleva ambaye anatajwa kuupa msingi ambao sasa unatoa ajira kwa mamilioni ya watu wa rika mbalimbali.

 

Dully au Mr Misifa aliyezaliwa Disemba 4, 1980 jijini Dar, wiki ijayo anatimiza umri wa miaka 39, lakini ukikutana naye utadhani ndiyo kwanza anaanza gemu la Bongo Fleva kutokana na mwili wake kutobadilika sana tangu alipoanza muziki miaka ya 2000.

 

Katika exclusive interview na Over Ze Weekend ya Gazeti la Ijumaa Wikienda, Dully au Mr Chicks anatoboa siri ya kutozeeka kwake kwamba, hali hiyo imetokana na kutopaka mafuta mwilini mwake tangu akiwa mdogo!

 

Baadhi ya ngoma kali za Dully zilizotamba ni pamoja na Salome, Handsome, Hi, Bijou, Nyambizi, Mtoto wa Kariakoo, Bongo Fleva, Utamu, Inde na nyingine kibao;

 

Over Ze Weekend: Kwanza hongera kwa kuwa mmoja wa majaji wa BSS 2019!

Dully: Asante, sisi ndiyo wakongwe wenyewe na tukikaa kwenye vitu kama hivi ndiyo eneo letu la kujidai.

Over Ze Weekend: Baadhi ya mamilioni ya mashabiki wako ndani na nje ya Bongo, wanasema tangu wameanza kukuona uko hivyohivyo kwa maana kwamba huzeeki, nini siri ya mafanikio?

 

Dully: Leo nitawaeleza siri yangu kubwa, mimi huwa situmii au sijipaki kabisa mafuta kwenye mwili wangu kwa miaka yote tangu nikiwa mdogo. Mimi nikishaoga nakuwa nimemaliza.

Over Ze Weekend: Vipi upande wa vyakula?

Dully: Siwezi kula chochote bila mboga za majani. Hata kama ninakula mihogo asubuhi au chakula kingine hasa vyakula vya baharini ambavyo ndivyo ninapendelea, siwezi kukosa mboga za majani.

 

Over Ze Weekend: Jina la Handsome ulijipa mwenyewe au ulipewa na nani na kwa nini?

Dully: Handsome nilipewa na marehemu Amina Chifupa. Nakumbuka nilipokutana naye enzi hizo akiwa na DJ Steve B kwa mara ya kwanza ndiyo walinipa jina hilo kwa sababu nilikuwa mdogo, halafu mzuri.

 

Over Ze Weekend: Sasa hivi jina lako moja la Mr Misifa hulitumii sana, kwa nini?

Dully: Unajua unavyoendelea kukua na majina mengine unayaacha maana kipindi kile nilikuwa na misifa na kila nikipita sehemu wadada walikuwa wanasema nina misifa, lakini sasa mambo yamebadilika, nimekua japokuwa watu wanasema bado umbo na sura ni ileile ya utotoni.

 

Over Ze Weekend: Kwa nini hupendi kuoa?

Dully: Kusema kweli kwenye akili yangu bado sijafikiria kabisa kuoa. Nataka kuoa muda ukifika, siyo kuchukua mwanamke anilindie nyumba!

Over Ze Weekend: Msomaji wetu angetamani kufahamu una watoto wangapi?

 

Dully: Nina watoto watano, wa kike watatu na wa kiume wawili. Wa kwanza ana umri wa miaka 15, wawili wana miaka 12, mwingine 10 na wa mwisho ana umri wa miaka saba.

Over Ze Weekend: Wote umezaa na mwanamke mmoja?

Dully: Hapana, kila mmoja ana mama yake.

 

Over Ze Weekend: Imekuwaje kila mmoja akawa na mama yake? Unaonekana ulikuwa hatari sana!

Dully: Sidhani kama wanawake wote walioolewa na waume zao ndiyo wameanza nao na mimi ndivyo ilivyotokea hadi nikawa na watoto hawa kwa mama tofauti.

Over Ze Weekend: Watoto wako hao unapata nafasi ya kukaa nao wote?

 

Dully: Ndiyo, wakifunga shule kila wakati wanakuja nyumbani ingawa mama zao wengine hawajuani kabisa.

Over Ze Weekend: Unapopata nafasi ya kukaa na watoto wako wote unawaambia nini?

Dully: Huwa ninawafundisha upendo, yaani kila mmoja amheshimu mwenzake.

Over Ze Weekend: Watoto wako wote unawapa mahitaji yao?

 

Dully: Ndiyo na ndiyo maana watu hawaoni mafanikio yangu kwa sababu nimewekeza kwa watoto wangu, huo ndiyo utajiri wangu.

Over Ze Weekend: Kuna mtoto wako yeyote anafuata nyayo zako?

 

Dully: Ndiyo, yupo, anaitwa Torano na tayari WCB (Wasafi Classic Baby) wamemchukua, wanasubiri tu amalize masomo.

Over Ze Weekend: Miongoni mwa mama zao kuna yeyote una mpango wa kumuoa?

Dully: Hapana.

 

Over Ze Weekend: Najua hadi sasa hujaoa, watoto wakija nyumbani kwako nani anawapikia au kuwafanyia vitu kama watoto?

Dully: Pale nyumbani kuna dada na mama yangu, hakuna shida kabisa.

MAKALA: IMELDA MTEMA

Comments are closed.