The House of Favourite Newspapers

Dully Sykes Afichua Siri kwa Nini Hafungi Ndoa!

0

UNAPOZUNGUMZIA wakongwe kwenye Bongo Fleva, basi unamaanisha wasanii kama Pince Dully Sykes. Mkongwe huyu licha ya kuanza gemu kitambo, bado ameendelea kulisimamisha jina lake kwenye ramani miaka nenda rudi.

 

Yes, Abdul Sykes amefanya mahojiano na Mikito Nusunusu, ambapo ameeleza mengi ambayo kwa namna moja au nyingine, pengine hujayasikia. Karibu:

MIKITO: Naona huzeeki bro kila siku unazidi kuwa kijana, nini siri yako bwana.

DULLY: Aahahah nshazeeka wewe…

 

MIKITO: Tumeona umekuwa ukitoa ngoma, tena kali kabisa, hebu tupe siri ya kuendelea kudumu kwenye muziki wako mpaka leo hii?

 

DULLY: Kutoboa ni kujielewa, kujiheshimu na kuheshimu wale wanaokufanya uwe pale, ila vijana wengi wa sasa wanapopata nafasi wanajisahau, mimi naomba tu niwaambie sio kwamba mimi natoa ngoma kali kuliko wote, hapana kuna watu wanatoa ngoma kali ila wanashindwa kutoboa kwa ajili ya tabia zao, wanatakiwa wajielewe kwanza na waishi kistaa kwa kufanya muziki wenye ladha tofauti tofauti.

 

MIKITO: Dully wewe ni mmoja kati ya wasanii ambao wana a.k.a nyingi sana, ila natamani utuambie Mr Misifa ilitokea wapi?

DULLY: Mr Misifa alinipa mama yangu mzazi, ila watu wengine ndiyo walilikuza baada ya kusikia mama ananiita Mr Misifa.

MIKITO: Kwa nini mama alipenda kukuita hivyo?

 

DULLY: Tangu nikiwa mdogo mimi napenda kuvaa vizuri, napenda kujisikia, juzi mama yangu alinipigia simu akasema tangu mtoto, mimi nilikuwa najipenda sana.

MIKITO: Kutoka Misifa’s Camp na sasa unataka kufungua record label yako, ndoto hiyo ulikuwa nayo tangu kitambo au imekuja tu siku za hivi karibuni?

 

DULLY: Ndoto ipo tangu muda tu, sema mara nyingi nakosa financial support na ndiyo maana nashindwa kuzifanya, nina ndoto nyingi sana nadhani tuombe Mungu, mambo mazuri yanakuja.

MIKITO: Unajua tukikuzungumzia, tunamzungumzia mtu mkubwa sana ambaye pia ni role model wa watu wengi, inakuwaje sasa unasema unapata shida kwenye masuala ya kifedha, ina maana unashindwa hata kuapproach watu wakupe msaada?

 

DULLY: Unajua ukipata au kuchukua pesa kutoka kwa mtu, huwezi kujua yule anayekupa ana lengo gani. Hivyo ni bora upambane tu utafute kwa jasho ufanye mambo yako. Nilishajaribu kuna kipindi, ila nikakosa msaada, ila nashukuru Mungu mimi kwa sasa namiliki vyombo vyangu full vya bendi, hata kipindi Koffi Olamide alipokuja kufanya show, vyombo vyangu ndiyo vilitumika pale Leaders Club.

 

MIKITO: Oktoba 9, 2018 inaonekana ni siku ambayo huwezi kuisahau mpaka ukaamua kuichorea tattoo mkononi?

DULLY: Ooh hapa nimeandika Pancho Latino, hii ni siku aliyofariki nadhani mnaelewa kwamba alikuwa ni kama mwanangu, mimi ndiyo nilimleta mjini na kazi zote za ki-producer. Katika studio yangu, alikuwa anazifanya yeye, pia nadhani alikuwa anapitia mambo mengi kabla hajafa ambayo yalimfanya akate tamaa kabisa ya kuishi.

 

MIKITO: Pole sana Dully, umeumia sana kwani ulikuwa mtu wake wa karibu sana zaidi ya ndugu, ila inaonekana alikosa washauri mpaka akakata tamaa, inakuwaje na wewe mtu wake wa karibu ulikuwepo?

DULLY: Hapana, kama ushauri nilikuwa nampa, lakini pia umauti unapokaribia kumfika mtu, anaona vitu vingi halafu isitoshe nilikuwa sikai naye, nadhani kilichobaki ni kumuombea tu.

 

MIKITO: Pia tunaona ni kwa muda sasa hujafanya nyimbo kwenye studio zako, shida nini?

DULLY: Kuna vitu tunarekebisha, vikikaa sawa studio yangu itafanya kazi kama kawaida, unajua studio yangu ina miaka kumi sasa, kwa hiyo kuna baadhi ya vifaa vimeshakuwa vya kizamani sana, hivyo tumeagiza nadhani soon vitafika.

 

MIKITO: Vipi kuhusiana na Record label yako unayokaribia kuianzisha, kuna wasanii tayari umesha-wasaini au kuna ambao unafikiria kuwaweka?

DULLY: Tayari kuna msanii nimeshamfikiria kutoka BSS sitaki kumtaja, ila anatokea Arusha na kuna mwingine anaitwa Corny nadhani mtamjua siku zikifika.

 

MIKITO: Ngoma yako mpya umemshirikisha Maua Sama, kwa nini Maua na si mwingine?

DULLY: Maua ni familia yangu na namshukuru pia amenipa heshima, ameitendea haki sehemu yake.

 

MIKITO: Kwa nini mkongwe kama wewe hujaoa?

DULLY: Ndoa sio kitu cha kawaida, unajua kwamba hata magonjwa mengi ya moyo yanasababishwa na ndoa, mimi najua kuna watu wapo kwenye ndoa, lakini wanatamani kuwa kama mimi.

 

MIKITO: Vipi kuhusu ukaribu wako na watu mliotoka wote kwenye gemu kitambo kama kina TID?

DULLY: Mimi sina tatizo na mtu, nipo nao vizuri wote washkaji zangu.

 

MIKITO: Lebo zipo nyingi sana sasa hivi, lakini tunaona na wewe unataka kuingia huko huko, unadhani utaweza kweli?

DULLY: Unajua hata wakati nafungua studio, niliambiwa mambo mengi lakini niliweza na nimefanikiwa kutoa nyimbo nyingi tu, kwa hiyo naamini itakuwa hivyo pia kwenye lebo.

 

MIKITO: Wewe ni msanii mkongwe lakini mpaka leo tunaona una tuzo mbili tu, tatizo nini?

DULLY: Sidhani kama hao wanaogawa tuzo wanakurupuka tu kusema tunamtaka mtu fulani kwenye tuzo, nadhani kuna vigezo vyao wanaangalia, pia wale waunganishaji wa tuzo wana watu wao.

 

MIKITO: Kuna chochote ambacho unaweza ku-share na mashabiki wako?

DULLY: Napenda kuwashukuru tu kwa sapoti yao na naomba waendelee kunisapoti.

MAKALA: ELIZABETH PHILIMIN

Leave A Reply