Dully Sykes akacha muziki
Hans Mloli, Dar es Salaam
MKONGWE wa Bongo Fleva, Dully Sykes ameamua kupumzika kufanya muziki kwa sasa na atakosekana kwa muda katika fani hiyo akidai kuwa yupo bize na mambo mengine yanayomzunguka.
Dully ambaye amedumu kwenye muziki kwa zaidi ya miaka 15, amewaeleza mashabiki wake kuwa wasitegemee chochote ndani ya mwaka huu labda anaweza kuufikiria tena muziki mara baada ya kumalizika kwa mwaka huu.
Dully aliyesikika mara ya mwisho kwenye Ngoma ya Confidence aliyoshirikishwa na T.I.D amesisitiza kukaa huko kando haitakuwa kwa upande wa kuimba bali hata kumsaidia mwanamuziki mwingine katika kazi zake.
“Sipo kabisa kwenye muziki kwa sasa, nimeamua kupumzika kwa sababu nipo bize sana na mambo yangu mengine, sitegemei kufanya chochote kwangu au kwa msanii mwingine kwa kitu kinachoitwa muziki, labda naweza kufikiria mwakani,” alisema Dully a.k.a Babydee.