The House of Favourite Newspapers

Dunia Ulioiacha Nyuma – 57

2

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.
Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.
Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.
Baadaye Magesa anagundua kwamba Grace ni jasusi wa kimataifa, akiwa amebadilisha jina na mwonekano wake, jambo linalompa hofu kubwa ndani ya moyo wake. Hata hivyo, msichana huyo anamuelewesha hali halisi.
Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi. Tayari baadhi ya mambo yameanza kufichuka ambapo inaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kifo cha Mwampashi na Magesa.
Kaburi ambalo kila mtu anaamini kwamba ndipo alipozikwa Magesa, linafukuliwa na sampuli zinachukuliwa kwa ajili ya vipimo vya DNA. Baadaye inabainika kwamba aliyezikwa hakuwa Magesa bali mtu mwingine tofauti kabisa.
Kadiri upelelezi unavyozidi kupamba moto ndivyo mambo mengi yanavyozidi kuibuka na sasa watu wengine wanahojiwa kuutafuta ukweli wa tukio zima. Sekretari wa Magesa na yule wa waziri mkuu nao wanahojiwa ambapo mambo ya ajabu yanazidi kubainika na sasa ipo wazi kwamba kuna mkono wa waziri mkuu.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Access Granted! Welcome! What can we help you?” (Umeruhusiwa! Karibu, tukusaidie nini?)
“May I speak in Swahili please!” (Naomba niongee kwa Kiswahili tafadhali) alisema mwanamke huyo kisha akabadili lugha na kuanza kuzungumza Kiswahili fasaha, jambo lililowafanya wote waliokuwa ndani ya chumba kile kutazamana.
“Najua mnaendelea na uchunguzi kuhusu sakata la Magesa na Mwampashi. Naomba mniunganishe na wanaohusika na uchunguzi wa sakata hilo, ninao mchango muhimu wa kuwapa,” alisema mwanamke huyo, wote wakatazamana tena.
Mmoja kati ya wale wanaume aliyeonekana kuwa na mamlaka kuliko mwenzake, aliinua mkonga wa simu na kuuweka sikioni, akaanza kuzungumza na upande wa pili kisha akawa anamuonesha ishara Mulisa ambayo mwenyewe aliielewa.
Akawa anabonyezabonyeza laptop yake na muda mfupi baadaye, skrini kubwa iliyokuwa kwenye chumba cha siri walikokuwa wamekaa maafisa watatu wa ngazi za juu katika idara ya usalama, Ephraim Mandiba, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, Pius Kasekwa, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali na Inspekta Jordan Ngai, Mkuu wa Upelelezi iliwaka na mwanamke yule akaanza kuzungumza moja kwa moja.
“Najua nyote hamnifahamu na kama yupo ambaye ananifahamu, atakuwa anaamini kwamba nimeshakufa lakini siyo kweli. Nipo hai na naendelea na majukumu yangu kama kawaida. Kwa msionifahamu, naitwa Grace, afisa kutoka Mossad ninayeshughulikia masuala ya Afrika,” alijitambulisha mwanamke huyo.
Mandiba alipomtazama tu, akili yake ilifanya kazi kwa kasi kubwa, akawa anajaribu kukumbuka amewahi kumuona wapi kwani sura yake haikuwa ngeni kwake lakini hakutaka kuonesha papara.
“Ndiyo Grace, mimi naitwa Ephraim Mandiba, mwenzangu hapa kushoto kwangu anaitwa Pius Kasekwa na huyu wa upande wa kulia anaitwa Jordan Ngai. Tumesikia unataka kuzungumza nasi kuhusu kesi tunayoishughulikia.”
“Ndiyo, nataka kuzungumza nanyi lakini nikizitazama sura zenu sioni kama kuna ujasiri wa kukabiliana na mhusika aliye nyuma ya haya yote. Najua tayari mnamjua lakini nani anaweza kuungana na mimi kuhakikisha tunamfikisha mbele ya sheria?”
“Unatutazama kwa wasiwasi Grace, lakini kabla hatujaenda mbali, tuambie kwa nini umeamua kutusaidia na kwa nini tukuamini.”
“Nataka kuwasaidia kwa sababu hiyo ni sehemu ya kazi yangu. Nimeshawasaidia wengine katika nchi mbalimbali kupambana na viongozi dhalimu wanaotumia vibaya madaraka yao. Lakini pia Magesa ni rafiki yangu wa siku nyingi, tulisoma pamoja kwa hiyo nina maslahi binafsi katika maisha yake.
“Kuhusu suala la kuniamini au kutoniamini, hilo nawaachia wenyewe,” alisema Grace kwa kujiamini wakati akizungumza kupitia njia ya kisasa ya mawasiliano ya Video Conference!
Wote walibaki kutazamana, Mandiba akainua mkonga wa simu na kumtaka Mulisa kuhakikisha kwamba mawasiliano hayo hayaonekani sehemu nyingine yoyote zaidi ya kwenye chumba walichokuwemo, harakaharaka akaanza kulishughulikia hilo na muda mfupi baadaye, kila kitu kilikamilika, wakawa wanazungumza wenyewe kwa usiri mkubwa.
“Kabla hatujaendelea, hebu itazame hii picha, unaweza kumtambua huyo mwanamke?” alisema Mandiba na kuigeuza laptop yake, akawa anaonesha moja kati ya zile picha alizopigwa Magesa akiwa chumbani na mwanamke, wote wakiwa watupu.
“Yaah! Huyo ni mimi na ndiyo maana kuanzia mwanzo nilishaeleza kwamba nina maslahi binafsi na Magesa. Ni mimi,” alisema Grace huku aibu za kikekike zikijidhihirisha wazi kwenye uso wake. Muda mfupi baadaye alivaa uso wa kazi na mazungumzo kuendelea.
“Mpaka sasa kuna utata mkubwa kama Magesa yupo hai au la! Unaweza kutuambia kuhusu hilo?”
“Magesa yupo hai na hapa nipo naye, anasikia kila tunachozungumza.”
“Tutaamini vipi?”
“Kabla ya kuwaaminisha, nataka mnihakikishie kwamba hakuna mtu mwingine yeyote atakayejua kuhusu hiki ninachoenda kuwaonesha.”
“Tunakuhakikishia, usiwe na wasiwasi,” alisema Mandiba, Grace akageuka na kuonesha ishara kama anazungumza na mtu. Muda mfupi baadaye, uso wa Magesa ulitokeza kwenye skrini, akiwa mzima, tena buheri wa afya, kila mtu akashtuka na kuanza kutazamana, wakiwa ni kama hawaamini.
“Hebu zungumza nao waamini kwamba kweli ni wewe,” alisema Grace, Magesa akawasabahi na kuwaambia kwamba hakuwa amekufa kama watu wote walivyokuwa wanaamini.
“Mungu wangu, ni yeye kweli,” alisema Mandiba huku akishindwa kuuficha mshtuko alioupata. Tangu aanze kazi yake miaka mingi iliyopita, alishawahi kukutana na matukio mengi ya ajabu lakini hilo lilionekana kuwa kiboko.
“Sasa Grace, unaweza kutuambia mko wapi kwa sasa?”
“Hapana, hilo swali siwezi kulijibu kwa sasa kwa sababu za kiusalama,” alisema Grace kisha mazungumzo yakaendelea.
Akawaambia mambo mengi ambayo hakuna aliyekuwa anayajua, kuanzia jinsi picha za Magesa na Grace zilivyopigwa wakiwa hotelini na aliyehusika na mchezo huo, jinsi Magesa alivyoliwa fedha nyingi kwa kutumia picha hizo, jinsi alivyonusurika kuuawa mara kadhaa, likiwemo tukio la kunusurika kwenye Msitu wa Kazimzumbwi.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne kwenye Gazeti la Uwazi

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

2 Comments
  1. Sylvester says

    mambo yanazid kunoga

  2. Elizabeth Mbuta says

    nzuri sana

Leave A Reply