Dunia Yamlilia Maradona

GWIJI wa zamani wa kandanda, Diego Maradona, amefariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 60 kwao Argentina ambapo mapema mwezi huu, Novemba, alifanyiwa upasuaji wa ubongo ambao madaktari walimwambia ulifanikiwa.
Baada ya kutangazwa kwa kifo hicho mastaa mbalimbali wamemlilia Maradona kupitia kwenye kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii, na Rais wa Argentina, Alberto Fernández, ametangaza siku tatu za maombolezo nchini humo.
Lionel Messi
Kwa upande wa Messi ambaye amekuwa mara kwa mara akilinganishwa na nyota huyo, alifanya kazi na Maradona wakati anaifundisha timu ya taifa ya Argentina wakat fainali za Kombe Dunia mwaka 2010 zilizofanyika Afrika ya Kusini. Kupitia mtando wa Instagram, Messi ameandika:

“Waargentina na dunia wanapita kwenye wakati mgumu sana. Diego ametutoka kimwili lakini anaishi ndani ya mioyo yetu, daima nitaendelea kuzienzi kumbumbuku zako, natanguliza salamu zangu za pole kwa familia na marafiki na wapenzi wote wa mpira wa miguu”.
Cristiano Ronaldo
Naye nyota wa timu ya taifa ya Ureno, Ronaldo amesema dunia imepoteza rafiki na mkali wa soka kuwahi kutokea. “Umeondoka mapema na pengo lako halizibika kamwe,” ameandika mtandaoni.

Pele
Mchawi wa soka kutoka Brazil, Pele, amesema amepoteza rafiki na lejendi wa soka na anaamini siku moja watacheza tena mpira mbinguni.

FC Barcelona
Klabu ya Barcelona imeandika kwenye mtandao: “Asante kwa kila kitu”. Maradona aliwahi kukipiga kwenye timu hiyo yenye maskani yake Catalunya.

Gary Lineker
Mmoja ya wachezaji waliokuwepo wakati Maradona anafunga kile kilichokuwa maarufu kwa kujulikana kama “bao la mkono” dhidi ya England ni Gary Lineker ambaye kwa sasa ni mtangazaji katika kituo cha runinga cha Sky Sports. Naye amemwelezea kama mchezaji bora katika kizazi chao wakati wanasakata kabumbu.

SSC Napoli
“Licha ya kupita katika vilabu kadhaa barani Ulaya. Timu ya Napoli ndipo palikuwa nyumbani kwake, na amepata mafanikio mengi akiwa hapa,” imeandika klabu hiyo mtandaoni.
Rasmi klabu hiyo imetangaza kuwa wataupa uwanja wao jina la Maradona kwa heshima ya gwiji huyo. Kwa sasa uwanja huo unaitwa San Paulo Stadium ukiwa ni wa tatu kwa ukubwa nchini humo baada ya Stadio Olimpico na San Siro. Una uwezo wa kuchukua watazamaji 55,000.


